Habari za Kitaifa

Charity Ngilu motoni kuhusu matumizi mabaya ya fedha za kiwanda cha nguo akiwa gavana

Na COLLINS OMULO August 30th, 2024 2 min read

HUENDA Gavana wa zamani wa Kitui Charity Ngilu akajipata pabaya, baada ya maswali kuibuliwa kuhusu matumizi ya fedha katika kiwanda cha kutengeneza nguo cha Kitui County Textile Center.

Haya yanajiri baada ya kamati ya Seneti kufuatilia matumizi ya fedha za umma, kumuagiza Bi Ngilu kufika mbele yake kujibu maswali kuhusu matumizi mabaya ya pesa za umma, katika kiwanda hicho, yaliyoibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu.

Maswali hayo yako katika ripoti ya matumizi ya fedha katika Kaunti ya Kitui katika miaka ya kifedha ya kati ya 2019 na 2022.

Kamati ya Seneti kuhusu Uwekezaji na Hazina Maalum, ilisema kuwa visa vya usimamizi mbaya wa fedha katika kiwanda hicho viliathiri utendakazi wake na uthabiti wake kifedha.

Hapo ndipo kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Vihiga, Bw Godffrey Osotsi ilimtaka Bi Ngilu kufika mbele yake kujibu maswali hayo.

Bw Osostsi, na wenzake, wanamtaka gavana huyo wa zamani kuandamana na waliokuwa wasimamizi katika kipindi husika (kati ya 2019 na 2022).

Bi Ngilu ambaye alihudumu kwa miaka mitano, kati ya 2017 na 2022, anatarajiwa kufika mbele ya kamati hiyo mwezi ujao, Septemba 2024.

Kamati hiyo ilimwita Bi Ngilu kwa misingi ya hitaji la Kipengele cha 125 cha Katiba na sehemu za 18 na 20 za Sheria kuhusu Mamlaka na Hadhi ya Bunge ya 2017.

Kipengele hicho cha Katiba kinalipa Bunge mamlaka ya kumwita mtu yeyote kufika mbele ili kutoa ushahidi au maelezo kuhusu suala linalochunguza.

“Ni kwa msingi huu ambapo tunamwagiza aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu, wasimamizi wakuu na maafisa wengine waliotia saini taarifa za kifedha za kiwanda cha Kitui County Textile Center katika miaka ya kifedha ya 2019/2020, 2020/2021 na 2021/2022,” akasema Bw Osotsi.

Gavana Julius Malombe ambaye alifika mbele ya kamati hiyo Jumatano, Agosti 28, 2024 anahitajika kuwasilisha ripoti ya Bodi ya Wakurugenzi kuhusu hali katika kiwanda hicho na maelezo mengine muhimu ndani ya siku tatu kabla ya siku ambayo Bi Ngilu atafika mbele yake.

Gavana huyo anahitajika kuwasilisha majina na anwani za wanachama wa Bodi ya Wakurugenzi waliosimamia kiwanda hicho katika kipindi cha uchunguzi.

“Aidha, Bw Malombe anapaswa kuwasilisha kwa kamati hii majina na maelezo kuhusu maafisa wakuu wa Serikali ya Kaunti ya Kitui walioketi katika bodi hiyo ndani ya siku tatu kabla ya kufanyika kwa mkutano huo,” akasema Bw Osotsi.

Kulingana na ripoti ya ukaguzi kuhusu matumizi ya fedha ya mwaka uliokamilika Juni 2022, mkaguzi aligundua dosari katika malipo ya Sh49.1 milioni kama mishahara kwa wafanyakazi vibarua.

Mkaguzi alitilia shaka viwango vya pesa vilivyolipwa.

Katika mwaka uliotanguliwa, kiwanda hicho kilimulikwa kuhusiana na malipo ya Sh56.7 milioni, ya mishahara kwa wafanyakazi vibarua ambao hawakuwa na mkataba.