Habari

COVID-19: Visa nchini Kenya vyapanda hadi 6,366

June 30th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

VISA jumla vya Covid-19 nchini vimefika 6,366 baada ya Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman kuthibitisha Jumanne visa 176 kutoka kwa sampuli 2,419 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Akitoa takwimu hizo katika Afya House, Dkt Aman amesema visa vyote 176 ni Wakenya.

Kati ya wagonjwa hao 100 ni jinsia ya kiume huku 76 wakiwa wa jinsia ya kike.

“Mgonjwa wa umri wa chini amekuwa na miaka 3, yule wa juu miaka 78,” Dkt Aman amesema katika kikao na wanahabari ambacho huandaliwa kila siku kueleza hali ya virusi vya corona nchini

Kaunti ya Nairobi imeandikisha maambukizi 99 katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Mombasa (20), Kiambu (17), Migori (13) na Uasin Gishu (10).

Aidha, Kajiado na Busia zimethibitisha visa vinne kila moja, Kilifi (3) na Machakos (2), huku Narok, Kisumu na Kakamega zikiwa na kisa kimoja kila kaunti.

Wizara imesema wagonjwa 26 wameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kuthibitishwa kupona Covid-19, Kenya ikiandikisha 2,039 idadi jumla ya waliopona.

“Vilevile tunasikitika kupoteza wagonjwa wanne zaidi, walioangamia kutokana na Covid-19, idadi jumla ya waliofariki ikifika 148 nchini ,” akasema.

Kufikia sasa, Kenya imekagua na kupima jumla ya sampuli 169,836

Na kuhusu wabunge, Spika Justin Muturi amesema ni wawili waliopata maambukizi ya Covid-19 akibainisha mmoja ameondoka hospitalini na sasa anajitenga kwake nyumbani.