Habari za Kitaifa

DCI yaahidi donge nono kwa atakayetoa habari kuwezesha Jumaisi kukamatwa

Na BENSON MATHEKA August 22nd, 2024 1 min read

IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeahidi zawadi ya pesa taslimu kwa mtu yeyote atakayetoa habari zitakazowezesha kumkamata mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake 42 ambao miili yao ilipatikana imetupwa kwenye timbo mtaani Kware, Embakasi, Kaunti ya Nairobi.

Collins Jumaisi Kalusha alitoroka kutoka seli za kituo cha polisi cha Gigiri Jumatatu, Agosti 20, 2024 pamoja na washukiwa wengine 12 raia wa Eritrea.

DCI ilisema kwamba Jumaisi anayetoka kata ndogo ya Shiru, Lokesheni ya Shaviringa, Kaunti ndogo ya Hamisi, Kaunti ya Vihiga alikuwa akisubiri kufunguliwa mashtaka ya mauaji lakini akatoroka kutoka seli za polisi.

“Zawadi ya kiasi kikubwa cha pesa itapatiwa yeyote aliye na habari za kuaminika zitakazosaidia kukamatwa kwake,” DCI inasema katika tangazo.

Walio na habari zozote kuhusu aliko wanaweza kuziwasilisha kwa siri kupitia laini ya #FichuaKwaDCI 0800722003 au kwa kupiga laini za simu za polisi 999, 911 na 112 au katika kituo chochote cha polisi kilicho karibu.

Jumaisi anadaiwa kukiri kuhusika na mauaji hayo ambayo baadaye yalipunguzwa kuwa ya wanawake sita.

Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi, Gilbert Masengeli alisema maafisa wanane waliokuwa kazini walisimamishwa kazi na kukamatwa kwa kusaidia mahabusu hao kutoroka.

Watano kati ya nane hao Jumatano, Agosti 21, 2024 walifikishwa katika Mahakama ya Milimani.

Polisi hao ni; Koplo Ronald Babo, Konstebo Evan Kipkirui, Konstebo Millicent Achieng, Konstebo Zachary Nyabuto na Konstebo Gerald Mutuku.