Akili MaliMakala

Dhana pamba ya kisasa inaharibu udongo na mimea ni porojo tu – NBA 

Na SAMMY WAWERU July 23rd, 2024 2 min read

KENYA ni kati ya nchi zinazokuza pamba ya kisasa ulimwenguni, ikisifiwa kutokana na ‘maumbile’ yake kustahimili athari za wadudu na magonjwa.

Isitoshe, inapigiwa upatu kufuatia uhimilivu wake kwa athari za tabianchi kama vile kiangazi.

Pamba hii maarufu kama Bt Cotton, iliidhinishwa kulimwa nchini 2018 baada ya Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bidhaa, ndiyo, National Biosafety Authority (NBA), chini ya Kifungu cha 2 cha Sheria ya 2009 kuhusu usalama wa Kibayolojia, kuridhishwa na utafiti uliofanyika.

Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro), ni mojawapo ya asasi za kiserikali zinazofanya utafiti wa mimea na mifugo nchini, na ukaguzi wa pamba iliyoboreshwa ulifanywa nalo kwa ushirikiano a wadauhusika wengine.

Mahindi na mihogo, yanaendelea kufanyiwa majaribio.

Hata licha ya pamba ya kisasa kusheheni tija, wakosoaji wake wanaitilia shaka pamoja na bidhaa zingine za kilimo ambazo jeni zake zimeboreshwa Kisayansi (GMO).

Dkt Roy Mugiira Afisa Mkuu Mtendaji Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bidhaa (NBA) akielezea kuhusu ukuzaji wa bt cotton pamoja na mbaazi kwenye shamba la mkulima Kirinyaga. PICHA|SAMMY WAWERU

Wanadai mimea ya GMO inapopandwa na mingine, inaiathiri pamoja na mazingira.

Hata hivyo, kulingana na NBA ‘hiyo ni dhana potovu inayoendeshwa na wanasiasa’.

“Kwa mfano, tumebaini kuwa bt cotton haina madhara yoyote kwa mazingira, binadamu, wanyama na hata mimea,” anasema Dkt Roy Mugiira, Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka hiyo.

Pamba iliyoboreshwa ilianza kukuzwa karibu miaka 30 iliyopita, na mazao yake yanatumika kuunda mavazi na chakula cha mifugo.

Cotton seed cake ni masalia ya mbegu baada ya pamba kusindikwa, mafuta kumiminwa na kupondwapondwa, yanayogeuzwa kuwa malighafi ya utengenezaji malisho ya mifugo na fatalaizahai.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bidhaa (NBA), Dkt Roy Mugiira wakati wa mahojiano katika shamba la mkulima wa pamba ya kisasa Kaunti ya Kirinyaga. PICHA|SAMMY WAWERU

Yanatajwa kusheheni madini ya wanga, protini, Vitamini, fiber na Phosphorous.

Evans Ngure ni mmoja wa wakulima wa bt cotton katika Kaunti ya Kirinyaga, na wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa kuhusu Bioanuwai mwaka huu, alidokeza kwamba yeye hulima zao hilo pamoja na mimea mingine.

Siku hii maalum huadhimishwa Mei 22 kila mwaka, na kongamano la 2024 liliandaliwa na Open Forum on Agricultural Biotechnology (OFAB Kenya) kwa ushirikiano na International Service for the Acquisition of Agri-biotech Applications (ISAAA) AfriCenter, na NBA katika Chuo Kikuu cha Embu.

“Hulima mahindi, mbaazi na maharagwe ya kawaida kwenye laini kati ya mipamba,” Ngure anadokeza.

Ni thibitisho ambayo Dkt Mugiira anasisitiza kuwa ni ishara bt cotton ni salama kwa mazingira.

“Pamba hii kukuzwa pamoja na mbaazi inaashiria kwamba ni salama kabisa, na tetesi tunazoskia kutoka kwa watu ni dhana potovu inayosakatwa na wanasiasa,” afisa huyo akaambia Akilimali wakati wa mahojiano shambani mwa Ngure.

Evans Ngure, mkulima Kirinyaga, akielezea kuhusu kilimo cha pamba. PICHA|SAMMY WAWERU

Mkulima huyo amepanda mbaazi kwenye nafasi kati ya mipamba.

“Tangu nikumbatie pamba ya kisasa miaka minne iliyopita, sijashuhudia athari zake,” Ngure akasema.

Amekuwa kwenye kilimo cha pamba kwa zaidi ya miaka 30.

Pamba asilia – ile ya kitambo ni kipenzi cha mdudu maarufu kama cotton bollworm.

Aidha, anatajwa kuwa mharibifu zaidi kwenye mazao.

“Kupitia ukuzaji wa pamba ya kisasa, idadi ya kunyunyizia dawa imepungua kutoka mara 12 hadi chini ya 4,” anasema Dkt Mugiira.

Kando na utafiti kuonyesha pamba hiyo ni salama kwa udongo, kiwango cha mazao kimeandikisha kuongezeka mara dufu kufuatia kupungua kwa athari.

Ngure, kwa mfano anasema kwenye ekari moja anayozalisha bt cotton huvuna wastani wa tani moja – juu kutoka kilo 300.

Mbaazi ikiendelea kukua na kunawiri pamoja na pamba ya kisasa shambani. PICHA|SAMMY WAWERU