Michezo

Difenda wa Ingwe Mike Kibwage kuondoka Desemba

October 16th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

Sasa ni wazi kwamba difenda wa AFC Leopards Mike Kibwage atabanduka kambini mwa mabingwa hao mara 13 wa KPL huku kandarasi yake ikitarajiwa kutamatika mwezi Desemba.

Mwanadimba huyo alijiunga na Ingwe misimu miwili iliyopita lakini juhudi za kuandaliwa kwa mazungumzo kuhusu kandarasi mpya kati ya ajenti wake na uongozi wa AFC Leopards zimekuwa zikigonga mwamba.

Kulingana na meneja wake Charles Korea Omondi, Kibwage amepokea ofa nyingi nzuri ndani na nje ya nchi na hana jingine ila kugura kambi ya Ingwe.

“AFC Leopards haijaweza kuwasilisha ofa yoyote ya kuvutia kwa mchezaji huyo. Ukweli mchungu ni kwamba hadi leo hawajaweza kulipa fedha za kumsaini ingawa alijiunga na timu hiyo miaka miwili iliyopita. Anahisi kwamba hawana shughuli naye wala hawamthamini,” akasema Korea.

“Tunapozungumza klabu mbili za KPL zimeonyesha nia ya kutaka huduma zake na nyingine pia kutoka Zambia zinamwania kama nzige hatari. Tunaendelea na mazungumzo ila ukweli ni kwamba Kibwage yupo tayari kuondoka,” akaongeza Korea ambaye enzi zake alivuma na kikosi cha Harambee Stars.

Kinda huyo ambaye amesakatia kikosi cha taifa cha vijana waliochini ya umri wa miaka 23 na Harambee Stars anatazamwa kama mojawapo wa walinzi wenye ukwasi wa talanta wanaoibukia.