Dimba

Arsenal, Marseille wavutana kuhusiana na bei ya Nketiah

Na MASHIRIKA August 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, Uingereza

ARSENAL na Marseille wamekataa kulegeza kamba katika mazungumzo yao kuhusu uhamisho wa Eddie Nketiah.

Mwanabunduki huyo anamezewa mate na klabu hiyo ya Ufaransa ambayo iko sokoni kutafuta straika baada ya Pierre-Emerick Aubameyang kujiunga na Al Qadsiah nchini Saudi Arabia.

Nketiah amesukumwa chini katika orodha ya mastraika Arsenal inapenda kutumia na hajaanza mechi tangu mwaka huu uanze.

Arsenal wako tayari kumuuza kabla ya soko kufungwa mwisho wa mwezi huu wakipata ofa nzuri, huku ripoti zikidai kuwa Marseille wangependelea kumsaini kwa mkopo kabla ya kumfanya kuwa wao kabisa mwisho wa msimu 2024-2025.

Hata hivyo, Arsenal wanasemekana hawana haraka ya kuuza Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye amewahi kuvutia Crystal Palace.

Nketiah alikuwa katika kikosi cha Arsenal kilichozuru Amerika mwezi Julai na alishiriki mechi zote tatu za kujifua dhidi ya Bournemouth, Manchester United na Liverpool.

Straika huyo angali na miaka mitatu katika kandarasi yake ugani Emirates inayoletea mshahara wa Sh16.5 milioni kila wiki. Arsenal wanaitisha Sh4.9 bilioni. Marseille wako tayari kutoa Sh2.8 bilioni.

Arsenal sasa wamerejea mjini London kutoka Amerika na wamepigwa jeki na Aaron Ramsdale, Bukayo Saka, David Raya na William Saliba.

Wanne hao walikuwa wameongezwa mapumziko baada ya mataifa yao kupiga hatua kubwa katika Kombe la Ulaya (Euro 2024) lililoandaliwa nchini Ujerumani mnamo Juni 14 hadi Julai 14. Wanatarajiwa kuanza mazoezi wikendi hii.

Vijana wa kocha Mikel Arteta wana michuano miwili ya kujipima nguvu dhidi ya mabingwa wa Ujerumani Bayer Leverkusen na Lyon wiki ijayo.

Mabingwa hao wa zamani wa Uingereza wamekuwa wakiimarisha kikosi tayari kwa msimu mpya watakaouanza dhidi ya Wolves mnamo Agosti 17.

Kandarasi ya mkopo ya kipa Raya kutoka Brentford ilifanywa ya kudumu baada ya ada ya Sh4.4 bilioni naye difenda Mwitaliano Riccardo Calafiori amejiunga kwa Sh6.9 bilioni kutoka Bologna.

Arsenal bado wako sokoni wakitafuta kusajili kiungo na mshambulizi. Wanamezea mate Mikel Merino kutoka Real Sociedad aliyeshinda Euro 2024 na timu yake ya Uhispania.

Merino anaingia katika mwaka wake wa mwisho na hajakuwa tayari kuongeza kandarasi yake.

Kuna tetesi kuwa Kieran Tierney, Reiss Nelson na Ramsdale wataondoka Emirates kabla ya soko kufungwa, lakini kutegemea ofa zitakazowekwa mezani.