Kompyuta ya Opta yaondoa Man City na Arsenal kwenye hesabu, yawekea Liverpool ‘kichwa’
LIVERPOOL, Uingereza.
Msimu 2024-2025 ukianza Agosti 16, Liverpool walikuwa na uwezo wa asilimia 5.1 wa kutawala Ligi Kuu ya Uingereza.
Katika ubashiri wa kompyuta maalum ya Opta, vijana wa Arne Slot walifuata mabingwa watetezi Manchester City (asilimia 82.2) na Arsenal (12.2) na kuwa mbele ya Chelsea (0.2) na Newcastle United (0.1).
Hata hivyo, baada ya kusakata mechi 18, Opta sasa imetoa City na Arsenal kwenye hesabu ya kushinda ligi, na kuwekea Liverpool ‘kichwa’.
Liverpool maarufu kama Reds, wameonyesha ni moto wa kuotea mbali na kuwa wako pazuri zaidi kuwa mabingwa wa ligi hiyo ya klabu 20.
Kwa mujibu wa Opta, vijana wa Slot wana uwezo wa asilimia 87.8 wa kutawala ligi hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2020.
Dalili zinaonyesha haitakuwa rahisi kung’oa Liverpool kileleni. Wamefungua mwanya wa alama nane dhidi ya wapinzani wa karibu, sapraizi Nottingham Forest ambao Opta ilibashiri wataponea tundu la sindano kushushwa ngazi kabla ya msimu kung’oa nanga.
Reds wanasakata soka ya kupendeza wakiongozwa na mshambulizi matata Mohamed Salah.
Raia huyo wa Misri amechangia katika kupatikana kwa magoli 30 katika michuano 18. Anaongoza ufungaji baada ya kucheka na nyavu mara 17 na kusuka asisti 13.
Katika ukatili wa hivi punde, Reds walibomoa West Ham 5-0 kupitia mabao ya Luis Diaz, Cody Gakpo, Salah, Trent Alexander-Arnold na Diogo Jota. Salah alichangia asisti za Gakpo na Jota.
Mbali na kutandaza soka nzuri, Liverpool pia wana bahati ya kutokuwa na majeraha mengi. Kwa sasa ni Conor Bradley na Ibrahima Konate wanakaribia kutoka chumba cha majeruhi baada ya kuwa nje majuma sita. Joe Gomez alipata jeraha dhidi ya West Ham.
Ukatili wa Liverpool unadhihirisha kuwa City ya Pep Guardiola inayokamata nafasi ya tano kwa alama 31 kutokana na mechi 19 na nambari tatu Arsenal (36) zitalazimika kufanya kazi ya ziada.
Mbali na Forest, Chelsea pia wamejitokeza kwa nguvu msimu huu.