Dawa ya kutibu Man United yatafutwa: Mrithi wa Ten Hag ni kati ya ‘wataalam’ hawa
PAMOJA na matokeo duni katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na West Ham United dhidi ya Manchester United mnamo Jumapili ugani London Stadium ulichochea zaidi kupigwa kalamu kwa kocha Erik ten Hag aliyetua Old Trafford mnamo Aprili 2022.
Kichapo hicho kiliteremsha mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi nafasi ya 14 jedwalini wakiwa na alama 11 huku pengo la pointi 12 likiwatenganisha na mabingwa watetezi Manchester City wanaoselelea kileleni. Ni matokeo yaliyoendeleza rekodi duni ya Man-United ambao sasa wameshinda michuano mitatu pekee kati ya tisa iliyopita ligini.
“Ipo haja kwa mambo kubadilishwa, kuanzia kwa mtazamo wa wachezaji hadi kwa mbinu za ukufunzi. Uthabiti wa kikosi umeshuka na ratiba ijayo ni ngumu,” akasema sogora wa zamani wa Man-United, Gary Neville mwishoni mwa mechi ya Jumapili.
“Iwapo lengo ni kurejesha hadhi ya kikosi na kuwa miongoni mwa wawaniaji wakuu wa ufalme wa EPL na makombe mengine bara Ulaya, basi kufutwa kwa Ten Hag ni suala la ni lini, si la iwapo,” akaongeza.
Kauli hiyo ilikoleza tetesi kuwa mabosi wa Man-United wamekuwa wakizungumza kisiri na baadhi ya wakufunzi wanaopigiwa upatu kumrithi Ten Hag aliyeshuka dimbani dhidi ya West Ham dalili zote zikiashiria kwamba alikuwa na siku za kuhesabika Old Trafford.
Mnamo Julai, Man-United walirefusha mkataba wa Ten Hag, 54, hadi Juni 2026 licha ya kumfanyia mahojiano ya kazi mkufunzi Thomas Tuchel aliyeajiriwa na timu ya taifa ya Uingereza. Man-United tayari wamerejea sokoni kusaka kocha mpya atakayejaza pengo la Ten Hag ambaye ni mkufunzi wa nane kuhudumu Old Trafford tangu Sir Alex Ferguson astaafu 2013. Wanaposubiri mchakato huo kukamilika, Ruud van Nistelrooy ambaye alikuwa msaidizi wa Ten Hag, atashikilia mikoba.
Inadaiwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Man-United, Omar Berrada, ameelekea Uhispania kushawishi kocha wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez, kujaza pengo la Ten Hag. Wakufunzi wengine wanaohusishwa na nafasi hiyo ni Graham Potter, Ruben Amorim wa Sporting Lisbon, Thomas Frank wa Brentford, kocha wa zamani wa Borussia Dortmund Edin Terzic, aliyekuwa kocha wa Uingereza Gareth Southgate.
Tangu 2013, makocha ambao wamenoa Man-United ni David Moyes, Ryan Giggs, Louis van Gaal, Jose Mourinho, Ole Gunnar Solskjaer, Michael Carrick na Ralf Rangnick. Miamba hao walimwaga sokoni zaidi ya Sh98 bilioni kwa ajili ya kujisuka upya kuanzia 2022-23 huku Ten Hag akijinasia huduma za Leny Yoro, Manuel Ugarte, Matthijs de Ligt, Joshua Zirkzee na Noussair Mazraou msimu huu.
Roy Keane na Paul Scholes ambao ni wanasoka wa zamani wa Man-United wamesema miamba hao wa zamani wana ulazima wa “kubadilisha mbinu zao za kutandaza soka” iwapo wana ndoto ya kujinyanyua, kuanza kuwika tena na kuwa miongoni mwa wagombeaji halisi wa taji la EPL.
Man-United kwa sasa wanakamata nafasi ya 21 kwenye hatua ya makundi ya Europa League kwa alama tatu kutokana na mechi tatu. Watavaana kesho na Leicester City katika Carabao Cup kabla ya kualika Chelsea kwa gozi kali la EPL wikendi hii.