Dimba

Guardiola: Sina ‘stress’, ninachojua ni kwamba Man City itafufuka na kuumiza upinzani

Na TOTO AREGE, MASHIRIKA December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, UINGEREZA

NYAKATI zimekuwa ngumu kwa Manchester City chini ya Pep Guardiola, lakini kumekuwa na hisia kwamba wataamka na watakuwa sawa huko mbele.

Mashine ya City inaonekana imevunjika, udhibiti ambao umewaendesha kwa muda mrefu haupo, umekwenda. Walipata kipigo kingine, cha sita katika mechi saba za mashindano yote. Ni wazi sasa kwamba, itakuwa ni vigumu kwao kutetea taji.

Umati wa mashabiki wa Liverpool ulimjulisha Guardiola kwamba, atatimuliwa asubuhi, jambo ambalo lilimfanya kuwakumbusha kwa kuinua vidole sita kuashiria kiasi cha mataji ya Ligi ya Premia ambayo ameshinda tangia alipofika Etihad mwaka 2016.

Ushindi huo mkubwa wa Liverpool wa 2-0 dhidi City Jumapili usiku ugani Anfield, ulifungua mwanya wa alama tisa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mabao hayo yakitiwa kimiani na wing’a Cody Gakpo na kiungo Mohammed Salah dakika ya 12 na 78 kupitia penalti mtawalia.

Kipigo cha City kimewafanya kuporomoka hadi nafasi ya tano chini ya Brighton & Hove Albion wakiwa na alama sawa (23).

Baada ya mechi 13, ‘Kompyuta bora’ ya Opta inaipa Liverpool nafasi ya 85.1% ya kunyanyua taji lao la 20 la EPL la hivi maajuzi wakiwa wameshinda taji hilo msimu wa 2019/20 chini ya kocha wa zamani Jurgen Klopp.

“Ni nafasi nzuri kuwamo,” alisema kocha wa mpya wa Liverpool Arne Slot baada ya mechi hiyo.

“Nyinyi mnajua zaidi kuliko mimi kwamba Arsenal na City wanaweza kushinda kila mechi kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu. Chelsea wanaweza kushinda kila mechi. Inaifanya EPL kuwa ya kuvutia sana.”

“Msimu uliopita kulikuwa na tofauti kubwa ya pointi kati ya Arsenal na City na bado waliweza kurejea mchezoni na kutwaa ubingwa.”

Arsenal ambao walimaliza nafasi ya pili nyuma ya City kwa misimu miwili iliyopita, pamoja na Chelsea wanafanya vyema zaidi msimu huu kuliko ilivyotarajiwa chini ya Enzo Maresca – wanashika nafasi ya tatu na alama sawa (23).

Lakini je, kushinda mataji sita ya kunamfanya Guardiola aepuke kufutwa?

Guardiola pia alikiri kwamba huenda “anastahili kufukuzwa” baada ya mechi yake ya saba mfululizo bila ushindi.

“Matokeo yatatusaidia kuona zaidi, lazima niwaone wachezaji wakirudi na kuwa bora zaidi kimwili, ni ngumu katikati ya msimu kwa sababu hatuwezi kubadilika, ni jambo lingine na hatuwezi kutarajia zaidi ya hili.

Guardiola alisema anahitaji kutafuta suluhu ili kuwa imara.

“Lazima nitafute suluhu la kuwa imara, nyuma hasa. Wachezaji hawa wamenipa nafasi ya kuishi labda miaka bora zaidi ya maisha yangu.

“Ninachoweza kufanya ni kuwa hapa kujaribu kutafuta suluhu. Katika wakati mwafaka klabu itafanya uamuzi kuhusu kile kinachohitajika kuruhusu klabu hii kuwa bado ipo.”