Harambee yaipiga Zambia CHAN na kuepuka safari ya Tanzania
HARAMBEE Stars Jumapili ilitinga kileleni mwa Kundi A katika kipute cha Kombe la Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024) baada ya kuichapa Zambia 1-0 katika uga wa MISC Kasarani.
Mvamizi Ryan Ogam alifunga bao hilo dakika ya 75 na kuwaamisha mashabiki 27,000 ambao walikuwa Kasarani akiwemo Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga.
Kiungo Boniface Muchiri alikuwa amepokea pasi kutoka kulia, akaenda na mpira hadi katikati mwa uwanja na kuumegea Ogam ambaye hakuwa ameandamwa na mchezaji yoyote.
Sajili huyo mpya wa Gor Mahia aliudhibiti mpira na kuachilia fataki ambayo ilimlemea kipa wa Zambia kunyaka na kuamsha umati ambao ulikuwa unashangilia vijana wa nyumbani.
Ogam sasa amefunga mabao mawili ikizingatiwa pia alifunga katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Morocco Jumapili iliyopita. Kwa mara nyingine alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi baada ya kupata tuzo hiyo katika mechi ya Morocco pia.
Kabla ya bao hilo Harambee Stars walikuwa wamebisha sana langoni mwa Chipolopolo bila mafanikio.
Ushindi huo ulihakikisha Kenya inamaliza juu ya Kundi A kwa alama 10, na sasa itacheza robo fainali dhidi ya Madagascar Ijumaa hii hapa nchini.
Morocco ilimaliza nambari mbili katika kundi hilo baada ya kuitandika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) 4-1 katika mechi nyingine ugani Nyayo. Kenya ingecheza dhidi ya Tanzania iwapo haingeshinda mechi hiyo kwa kuwa wangemaliza nambari mbili kundi lao.
Angola walibanduliwa wakiwa na alama nne huku Zambia ikiwa haina alama zozote baada ya kupoteza mechi zake kundi A. Morocco sasa itacheza dhidi ya Tanzania ugenini kwenye mechi nyingine ya robo fainali baada ya kumaliza nambari mbili.
Ushindi huo pia umenufaisha wanasoka wa Harambee Stars kifedha kwa kuwa watapokea Sh2.5 milioni kwa kila mchezaji jinsi walivyoahidiwa na Rais William Ruto.