Hivi hawa Manchester United ni wateja wa ‘relegation’?
KOCHA Ruben Amorim, 40, amekiri kuwa kibarua chake ni “kigumu sana” baada ya waajiri wake Manchester United kukubali kichapo cha 1-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur na hivyo kuachwa katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Mkufunzi huyo raia wa Ureno alishuhudia Red Devils wakitandikwa kwa mara ya nane kutokana na michuano 12 ya EPL huku bao la kiungo James Maddison katika dakika ya 13 likiwapa Spurs ushindi muhimu.
Kwa mara nyingine, Man-United walionekana kuzidiwa ujanja katika takriban kila idara ingawa Amorim alikosa huduma za masogora 12 tegemeo kutokana na majeraha na hivyo akalazimika kuweka benchi idadi kubwa ya wanasoka chipukizi.
Amorim, ambaye mara nyingi ameshindwa kudhibiti hisia zake kila anapohojiwa na wanahabari mwishoni mwa mechi aliyopoteza, alisema: “Nina matatizo mengi. Kazi yangu ni ngumu sana lakini nipo hapa kuiendeleza kila siku na kila wiki kwa imani kwamba nitajaribu kukifufua kikosi na tuanze tena kushinda michuano.”
Licha ya Man-United kuwa chini kwa zaidi ya dakika 70, Amorim hakufanyia kikosi chake mabadiliko yoyote hadi mwishoni mwa kipindi cha pili alipomleta ugani tineja Chido Obi, 17.
Fowadi huyo alikuwa miongoni mwa makinda wanane waliopangwa benchi na Amorim ambaye ameapa kusuka upya kikosi chake katika kipindi cha miezi michache ijayo japo dalili zote zinaashiria kuwa siku zake ugani Old Trafford ni za kuhesabika tu.
“Kipute cha EPL ndicho kigumu zaidi duniani. Ninajaribu kuwa makini na chipukizi hawa. Nilihisi timu ikiwa na ari ya kusawazisha na sikutaka kutatiza azma hiyo kwa mabadiliko mengine. Ingawa wote wasingewajibishwa dhidi ya Spurs, kila mmoja wao atapata fursa ya kucheza na kudhihirisha uwezo wake uwanjani,” akasema Amorim.
“Nipo hapa kusaidia wachezaji wangu. Ninaelewa ugumu wa hali yangu. Ninajiamini katika kazi yangu na ninataka kuanza kushinda kila mechi. Nafasi yetu kwenye msimamo wa jedwali inanipa wasiwasi. Pengo la alama kati yetu na viongozi linazidi kuongezeka na tunakaribia sana mkia wa jedwali.”
“Ipo haja kwa mambo kubadilishwa, hasa kuanzia kwa mtazamo wa wachezaji kwa sababu hatuwezi kubadili mbinu za ukufunzi kila mara. Iwapo lengo ni kurejesha hadhi ya kikosi na kuwa tena miongoni mwa wawaniaji wakuu wa ufalme wa EPL na makombe mengine ya Uingereza na bara Ulaya, basi hali si shwari kwa sasa. Hofu zaidi ni kuwa uthabiti wa kikosi umeshuka na ratiba ijayo ni ngumu,” akaeleza.
Mbali na kumzidishia Amorim presha ya kupigwa kalamu, kichapo kutoka kwa Spurs pia kiliendeleza rekodi duni ya Man-United ambao wamepoteza mechi 13 kutokana na mashindano yote kufikia sasa msimu huu na tisa tangu Mreno huyo atue Old Trafford mnamo Novemba 2024.
Man-United wameshindwa mara 12 kutokana na michuano 25 iliyopita (W8 D5), hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi ya mechi ambazo wamepoteza kutokana na 25 za mwanzo wa msimu tangu 1973-74 (13), waliposhushwa daraja mara ya mwisho katika EPL.
Kwa kupoteza mechi nane kati ya 12 zilizopita, Man-United wanaingia katika kundi moja na Leicester City (tisa) na Southampton (10) – timu zinazoshikilia nafasi mbili za mwisho jedwalini baada ya kupokezwa vichapo vingi zaidi ligini kufikia sasa.
Ni Leicester (saba) pekee ambao wamefunga mabao machache zaidi katika kipindi cha kwanza kuliko Man-United (tisa) muhula huu.
Red Devils wametikisa nyavu za wapinzani mara moja pekee katika kipindi cha kwanza kutokana na mechi 10 zilizopita – penalti ya nahodha Bruno Fernandes dhidi ya Brighton mnamo Januari.
Beki wa zamani wa Man-United, Gary Neville, anahisi kumekuwa na dalili ndogo sana ya mambo kuimarika kambini mwa kikosi hicho tangu Amorim apokezwe mikoba ambayo kocha Erik ten Hag alipokonywa Novemba mwaka jana.
“Ingawa klabu ina uhaba wa wachezaji bora na italazimika kuwa na subira, ningependa kuona viwango vya utendaji vikiimarika. Kiwango cha sasa cha mchezo wa Man-United ni cha wastani mno,” akasema Neville.
Ushindi wa Spurs dhidi ya Man-United ulikuwa wao wa kwanza baada ya mechi tatu huku wakidenguliwa pia kwenye vipute viwili ndani ya kipindi cha siku nne.
Kichapo cha 2-1 kutoka kwa Aston Villa katika Kombe la FA ugenini, siku nne baada ya kung’olewa na Liverpool katika Carabao Cup kwa jumla ya mabao 4-1, kilizima ghafla ndoto ya Spurs ya kukomesha ukame wa miaka 17 wa mataji kabatini mwao.
Matokeo hayo duni yaliendeleza masaibu ya kocha Ange Postecoglou na kuning’iniza pembamba hatima yake katika kambi ya miamba hao wa London Kaskazini.
Spurs sasa wameshinda mechi nne kati ya 12 zilizopita katika mashindano yote na wanakamata nafasi ya 12 kwenye jedwali la EPL kwa alama 30 sawa na Crystal Palace na Everton. Wako juu ya Man-United kwa pointi moja pekee.