Dimba

Isak hatimaye afuta nuksi ya kutofungia Liverpool kwenye EPL wakizoa ushindi muhimu

Na GEOFFREY ANENE December 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SAJILI ghali kabisa katika historia ya soka ya Uingereza, Alexander Isak, hatimaye amepata bao kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2025-2026 ulioanza Agosti 16, 2025.

Isak alifuma wavuni bao safi kutokana na asisti ya Cody Gakpo dakika ya 60 katika ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji West Ham hapo Jumapili, Novemba 30, 2025. Gakpo alifunga bao la pili dakika za majeruhi.

West Ham walikamilisha mechi hiyo wakiwa watu 10 baada ya Lucas Paqueta kulishwa kadi nyekundu dakika ya 84.

Kabla ya bao raia huyo Mswidi mwenye asili ya Eritrea alikuwa ameona lango mara moja tu – dhidi ya Southampton katika Kombe la Carabao mnamo Septemba 23 ugani Anfield.

Isak aliingia mechi dhidi ya West Ham pia akiwa ameonja ushindi mara moja tu ligini ambao ulikuwa wakati Liverpool walipepeta majirani Everton 2-1 hapo Septemba 20.

Isak (kulia) amsalimu kocha wake Arne Slot alipoondolewa wakati wa mechi dhidi ya West Ham. PICHA | REUTERS

Tangu ushindi dhidi ya Everton, Isak alikuwa amepoteza michuano minne mfululizo ya ligi ambayo ameanzishwa na hivyo kumfanya kuwa mchezaji wa kwanza kupata historia hiyo tangu Percy Saul mwaka 1906.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 26 amenufaika kuanzishwa na kocha Arne Slot baada ya mvamizi matata wa Misri, Mohamed Salah, kutiwa benchi Jumapili.

Ushindi dhidi ya West Ham umewezesha Liverpool kuingia mduara wa 10-bora kutoka nafasi ya 13 hadi nane. Mabingwa hao watetezi wana alama 21 baada ya mechi 13 za kwanza.

Isak alinunuliwa na Liverpool kwa Sh21.37 bilioni kutoka Newcastle United hapo Septemba 1, 2025. Hiyo ilikuwa siku chache tu baada ya Liverpool kuvunja rekodi ya uhamisho ikinunua Florian Wirtz kutoka Bayer Leverkusen kwa Sh18.7m.