Liverpool yaiponda Arsenal kocha Arteta akikemea vijana wake kwa kukosa kuwa katili
KOCHA Mikel Arteta ameelezea wasiwasi wake kuwa vijana wake wanafaa kuwa katili zaidi langoni baada ya kukamilisha ziara ya Amerika kwa kupoteza 2-1 mikononi mwa Liverpool Alhamisi.
Wanabunduki wa Arsenal walinyamazishwa na mabao kutoka kwa Mohamed Salah na Fabio Carvalho yaliyopatikana kutokana na pasi murwa kutoka kwa Harvey Elliot dakika ya 13 na 34 mtawalia.
Kai Havertz alifungia Arsenal bao la kufutia machozi dakika ya 40 baada ya kukamilisha kwa ustadi pasi safi kutoka kwa nahodha Martin Odegaard ugani Lincoln Financial Field.
Kabla ya mechi hiyo, ambayo Arteta hakuwatumia Jurrien Timber na sajili mpya Riccardo Calafiori, Arsenal walikuwa wametoka sare ya 1-1 dhidi ya Bournemouth na kulemea Manchester United 2-1.
“Bila shaka, tunaweza kuimarika. Matokeo yangekuwa tofauti kama tungetumia nafasi za kwanza vyema. Tulipata nafasi nyingine mbili ama tatu nzuri, lakini tukazipoteza,” akasema Mhispania huyo ambaye aliongoza Arsenal kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya pili mara mbili mfululizo nchini Uingereza.
Arsenal, ambao walishinda ligi mara ya mwisho msimu 2003-2004, wataalika mabingwa wa Ujerumani Leverkusen ugani Emirates Agosti 7 na kisha Lyon kutoka Ufaransa mnamo Agosti 11 katika mechi za kirafiki kabla ya kufungua msimu dhidi ya Wolves (Agosti 17).
Majeraha
Kwingineko, Manchester United ilipata pigo baada ya beki mpya Leny Yoro kuthibitishwa atakuwa mkekani kwa miezi mitatu tofauti na kipindi cha kati ya majuma matatu na sita ilivyodhaniwa.
Yoro aliyeumia kidole cha mguu dhidi ya Arsenal, anatarajiwa kuwa nje hadi Novemba. Mashetani hao Wekundu pia watakuwa bila mshambulizi Rasmus Hojlund kwa wiki sita.
Vijana wa kocha Erik ten Hag waliendeleza vyema matayarisho yao kwa kupepeta Real Betis kutoka Uhispania 3-2 uwanjani Snapdragon mjini San Diego nchini Amerika hapo jana.
United walipata mabao kupitia kwa Marcus Rashford (penalti), Amad Diallo na Casemiro nao Betis wakajifariji kwa magoli kutoka kwa Iker Losada na Diego Llorente.
Timu ya United, ambayo pia ina hofu kuhusu jeraha la mchezaji Antony, itakamilisha ziara ya Amerika dhidi ya Liverpool ugani Williams-Brice mnamo Agosti 4.
Chelsea nao walipata ushindi wao wa kwanza katika mechi za kujiandaa kwa msimu mpya baada ya kukung’uta Club America kutoka Mexico 3-0 kupitia mabao ya Christopher Nkunku (penalti), Marc Guiu na Noni Madueke (penalti) ugani Mercedes-Benz mjini Atlanta, Alhamisi.
Vijana wa kocha Enzo Maresca walitoka 2-2 dhidi ya Wrexham na kupoteza 4-1 dhidi ya Celtic katika mechi mbili za kwanza.
Watamenyana na Manchester City (Agosti 4), Real Madrid (Agosti 7) na Inter Milan (Agosti 11) katika mechi za kirafiki kabla ya kuanza msimu dhidi ya City (Agosti 18).
katika mechi nyingine ya kujipima nguvu, Samuel Chukueze alifungia Inter Milan bao la pekee walipozima Real Madrid 1-0 jijini Illinois, Amerika hapo jana.