Man United waumiza nyasi bure dhidi ya Villa, Chelsea nao wakaziwa na Nottingham
BIRMINGHAM, Uingereza
MANCHESTER United waliumiza nyasi bure katika sare ya 0-0 licha ya kuendeleza rekodi yao nzuri ya kutopoteza dhidi ya wenyeji Aston Villa hadi mechi 25 kati ya 26 zilizopita ugani Villa Park mnamo Jumapili, Oktoba 6, 2024.
Katika idadi hiyo ya mechi, Villa, ambao walikuwa wamepigiwa upatu kuzima United, wana ushindi mmoja (3-1 Novemba 2022), sare tisa na wamepokea vichapo mara 16 ugani Villa Park.
United, ambao kocha wao Erik ten Hag anakabiliwa na hatari ya kufutwa kazi kutokana na matokeo duni, pia wangefikia rekodi ya ushindi mara nyingi dhidi ya mpinzani mmoja ligini ambayo kwa sasa ni 41 dhidi ya Everton. Mashetani hao wekundu wamepepeta Villa mara 40.
Hapo Jumapili, Villa walipata pigo mapema baada ya beki Ezri Konsa kujeruhiwa dakika ya 12 na nafasi yake ikajazwa na Diego Carlos. Kila pande ilijitahidi kufanya mashambulizi, lakini hakuna aliyeona lango katika dakika 45 za kwanza.
United walijaza nafasi ya beki Noussair Mazraoui mwanzo wa kipindi cha pili kwa kumuingiza Victor Lindelof dakika ya 46. Hata hivyo, walipata pigo sekunde chache baadaye baada ya beki Harry Maguire kupata jeraha, huku Ten Hag akiingiza Matthijs de Ligt katika nafasi yake.
Mechi ilizidi kuwa ya nipe-nikupe, huku kipa wa Villa, Emilio Martinez akafanya kazi ya ziada kuondosha kiki la mbali kutoka kwa Marcus Rashford dakika ya 48 naye Andre Onana akapangua shuti moto kutoka kwa Youri Tielemans dakika nane baadaye.
Rashford alilishwa kadi ya njano dakika moja baadaye kwa kumvyoga Matty Cash. Mshambulizi Jhon Duran, ambaye amekuwa akifungia Villa mabao muhimu kila akitokea kwa benchi, aliingia nafasi ya Leon Bailey dakika ya 63.
United walifanya mabadiliko mawili dakika moja baadaye kwa kuingiza washambulizi Joshua Zirkzee na Antony katika nafasi ya Rasmus Hojlund na Rashford, mtawalia. Nahodha Bruno Fernandes kisha alishuhudia frikiki yake ikigonga mwamba dakika ya 68.
Villa waliingiza Ian Maatsen katika nafasi ya Lucas Digne nao United wakapumzisha Kobbie Mainoo na kumingiza Casemiro dakika ya 85. Licha ya mabadiliko hayo dakika 90 pamoja na nane za majeruhi zilitamatika bila bao.
Katika mchuano mwingine Jumapili, wenyeji Chelsea walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Nottingham Forest ugani Stamford Bridge. Vijana wa kocha Enzo Maresca walijipata chini goli moja baada ya Chris Wood kutetemesha nyavu dakika ya 49. Hata hivyo, Blues walijikakamua na kusawazisha kupitia kwa Noni Madueke dakika nane baadaye.
Forest walisalia wachezaji 10 uwanjani baada ya James Ward-Prowse kulishwa kadi nyekundu dakika ya 78, lakini Blues hawakufanikiwa kutumia pengo hilo kupata bao la ushindi. Chelsea waliingia mchuano huo wakiwa wameshinda michuano mitano mfululizo katika mashindano yote.
Baada ya mechi saba za kwanza, Liverpool wanaongoza kwa alama 18 wakifuatiwa na mabingwa watetezi Manchester City (17), wanabunduki wa Arsenal (17), Chelsea (14), Villa (14), Newcastle (12) na Fulham (11). Nambari nane Tottenham Hotspur (alama 10) watasakata mechi yao ya saba baadaye Jumapili dhidi ya nambari 11 Brighton (alama tisa).
Manchester United wanapatikana katika nafasi ya 14 kwa alama nane.