Mbappe alivyozika Man City katika kaburi la sahau Klabu Bingwa Ulaya
NYON, USWISI
NYOTA Kylian Mbappe alimwaga kipa Ederson mara tatu katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Manchester City na kuisaidia Real Madrid kuweka hai matumaini ya kutetea taji lake la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kutinga 16-bora kwa jumla ya mabao 6-3, Jumatano.
Mbappe, ambaye sasa ana jumla ya magoli 27 msimu huu, alipata mabao yake ndani dakika 61. Nico Gonzalez alifungia City goli la kujiliwaza dakika za majeruhi.
PSV Eindhoven nao walibandua Juventus kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya kuduwaza miamba hao wa Italia 3-1 katika mechi ya marudiano nchini Uholanzi. Ryan Flamingo alifungia PSV bao la ushindi katika kipindi cha kwanza cha muda wa ziada.

Ivan Perisic aliweka PSV 1-0 dakika ya 53 kabla ya Timothy Weah kusawazishia Juve 1-1 dakika 10 baadaye. Sare ingetosha Juve kuingia 16-bora, lakini PSV walikuwa na mipango tofauti na kupata mabao zaidi kutoka kwa Ismael Saibari na Flamingo.
Timu hiyo ya Uholanzi imeshinda mechi ya muondoano ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 1-0 dhidi ya Arsenal mnamo Februari 2007.
Nao miamba wa Ufaransa, Paris Saint-Germain walituma onyo kwa wapinzani wao wa raundi ya 16-bora kwa kulipua Brest 7-0 katika mkondo wa pili kupitia mabao ya Bradley Barcola, Khvicha Kvaratskhelia, Vitinha, Desire Doue, Nuno Mendes, Goncalo Ramos na Senny Mayulu. Vijana wa Luis Enrique walipepeta Brest 3-0 katika mkondo wa kwanza.
Droo ya 16-bora ni Ijumaa
Dortmund wanakamilisha orodha ya washiriki wa mechi za 16-bora baada ya kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Sporting. Vijana wa Nico Kovac walitawala mkondo wa kwanza 3-0 nchini Ureno kabla ya kuumiza nyasi bure katika marudiano nchini Ujerumani.
Droo ya 16-bora itafanywa saa nane mchana leo ikihusisha Liverpool, Barcelona, Arsenal, Inter Milan, Atletico Madrid, Leverkusen, Lille na Aston Villa waliofuzu moja kwa moja kwa kumaliza msimu wa kawaida ndani ya nane-bora.
Nazo PSG, Real, Club Brugge, PSV, Feyenoord, Bayern Munich, Dortmund na Benfica zilijikatia tiketi kupitia mechi za muondoano za nambari tisa hadi 24.
Aidha, droo za kombe la Europa League na kipute cha Europa Conference League pia ni leo alasiri.