Rashford aendelea kung’aa Laliga
MARCUS Rashford kwa mara nyingine tena, alichangia ushindi wa Barcelona wa 3-1 dhidi ya Elche katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania Jumapili usiku ugani Estadi Olímpic Lluís Companys mjini Barcelona.
Kinda Lamine Yamal na Ferran Torres walifunga mabao mawili ya mapema dakika ya tisa na 11 kabla ya Rashford kufunga bao la tatu dakika ya 61 ya mchezo. Rafa Mir alifungia Elche bao la pekee dakika ya 42.
Hilo lilikuwa bao la pili la ligi la Rashford msimu huu na amechangia mabao matano.
Barcelona walilipiza kisasi baada ya kichapo cha 2-1 dhidi ya Real Madrid katika mechi ya ligi wiki moja iliyopita. Barca walipanda hadi nafasi ya pili, pointi tano nyuma ya vinara Real Madrid.
Sasa Barcelona ina rekodi ya mechi 25 bila kushindwa nyumbani wakiwa wameshinda 18 na kutoka sare saba.
Katika jedwali na wafungaji bora, mshambuliaji Kylian Mbappe wa Real Madrid amefunga mabao 13 katika mechi 11.
Katika matokeo mengine ya La Liga, Levante walipoteza 1-2 dhidi ya Celta Vigo, Alves wakavuna ushindi wa 2-1 dhidi ya Espanyol nao Real Betis wakaipepeta Mallorca 3-0.
Katika mechi za Ligi Kuu ya Italia ya Serie A, AC Milan walipata ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya AS Roma nao Inter Milan wakanyakua alama zote tatu kutokana na ushindi wa 2-1 dhidi ya Hellas Verona ugenini.