Dimba

Saka na Odegaard ndio wataifanya Arsenal kubeba taji la EPL – Wachanganuzi

Na MASHIRIKA December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WACHANGANUZI wa soka wasema matumaini ya Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) yatategemea mchango wa kiungo mshambulizi Martin Odegaard na fowadi Bukayo Saka ambao wamekuwa mafundi wakuu wa kikosi hicho tangu msimu uanze.

Arsenal ilipoteza fomu kwa majuma kadhaa mwezi jana wakati wawili hao walikuwa wakiuguza majereha, hususan nahodha Odegaard akiwa nje miezi miwili.

Hata hivyo, urejeo wa Odegaard umefufua makali ya masogora hao wa kocha MIkel Arteta ambao wanafagia timu kote kote — EPL na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kufuatia ushindi mwingine mnono Jumamosi, raundi hii West Ham wakitoa ndani 5-2, Arsenal ilichupa hadi nambari mbili na alama 25.  Mabao ya Arsenal yalitiwa kimiani na Gabriel Magalhães Trossard degaard Havertz Saka West Ham walijiliwaza kwa mabao ya Aaron Wan-Bissaka Emerson Palmieri

Gabriel Magalhaes (pili kushoto) asherehekea kufunga goli la kwanza la Arsenal dhidi ya West Ham, akiwa na Bukayo Saka (kulia) na Martin Odegaard (kushoto), Jumamosi. PICHA | REUTERS

Kusuasua kwa wapinzani wao wakuu Manchester City – ambao waliangushiwa kichapo tena EPL cha mabao 2-0 na vinara Liverpool ugani Anfield, Jumapili – kunawapa fursa nzuri zaidi vijana wa Arteta kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza tangu 2003.

Liverpool (alama 34) ndio timu pekee inaonekana kuwa tisho wa Gunners.

Kulingana na wachezaji wa zamani Jamie Frank Redknapp na Thomas Frank, ushindi dhidi ya West Ham hapo Jumamosi ni ishara tosha kwamba wanabunduki wa Arsenal wamerudi nari.

Kulingana na Frank, uwepo wa Odegaard na Saka unaongezea Arsenal nguvu zaidi. Timu haijapoteza mechi tangu mwezi April iwapo Odegaard yuko kikosini.

“Saka na Odegaard wanashirikiana vizuri na kufanya timu nzima ivutie,” alisema Redknapp aliyesakatia Liverpool na timu ya taifa Uingereza.

Frank akiunga kauli hiyo aliongeza: “Odegaard ndiye injini ya kikosi. Amefanya Saka avume zaidi. Arsenal inacheza boli ya kuvutia wakiwa kikosini.”

Saka akifunga penalti dhidi ya West Ham, Jumamosi. PICHA | REUTERS

Uwanjani London Stadium Saka alitoa asisti mbili katika mchuano huo pamoja na kufunga bao lake la penalti.

Mchango huo ulimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha asisti 10 katika ligi kuu tano za bara Ulaya msimu huu. Mchezaji anayemfuata ni Nuno Tavares na asisti nane akisakatia Lazio katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Itakumbukwa kuwa beki wa kushoto Tavares anachezea Lazio kwa mkopo kutoka Arsenal.

Isitoshe, penalti yake katika kipindi hicho cha kwanza ilimfanya Saka kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao na kutoa asisti katika mechi ya tatu mfululizo kwenye mashindano yote akivalia jezi ya Arsenal, tangu Cesc Fabregas afululize hivyo mechi nne mnamo Septemba 2007.

Saka alifunga goli na kutoa asisti katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Nottingham Forest kwenye EPL mnamo Novemba 23, 2024, kisha akafunga na kutoa asisti mbili Arsenal ilipogaragaza Sporting 5-1 mechi ya UEFA mnamo Novemba 26, 2024 kabla kushikilia uzi uo huo Jumamosi dhidi ya West Ham.