Dimba

Sasa farasi ni watatu KPL ikibaki mechi nne ligi ikamilike

Na CECIL ODONGO May 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBIO za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) huenda zikaamuliwa katika mechi nne za mwisho baada ya viongozi Kenya Police na Tusker kushinda mechi zao Wikendi.

Gor Mahia ambayo pia ipo kwenye kiny’ang’anyiro cha ubingwa pia haikuwa na mechi baada ya Debi ya Mashemeji kuahirishwa kutokana na ukosefu wa uwanja.

Uongozi wa Gor ulikataa pendekezo la kucheza uga wa Ulinzi Sports Complex bila mashabiki na sasa itabidi mchuano uchezwe tarahe nyingine kabla ya msimu huu wa KPL kukamilika mnamo Mei 30.

Kenya Police Ijumaa iliishinda Bandari 1-0 katika uga wa Mbaraki kupitia bao la dakika ya 91 la Marvin Nabwire.

Ushindi huo ulihakikisha wanaendelea kuwa kileleni kwa alama 58 wakiwa wamebaki na mechi nne msimu huu utamatike.

Tusker nao waliwapiga Murang’a Seal 2-0 kupitia mabao ya Eric Balecho na Mganda Deogratious Ojok katika uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos.

Ushindi huo ulipaisha Tusker hadi nafasi ya pili wakiwa na alama 55 kutokana na mechi 30. Gor ambayo imecheza mechi 29, ipo nambari tatu kwa alama 53.

Bao la Brian Eshihanda lilitosha kuhakikisha kuwa Kakamega Homeboyz wanashinda Mathare United 1-0 kwenye uwanja wa Dandaro.

Homeboyz wapo nafasi ya tano kwa alama 48, moja nyuma ya nambari nne Shabana ambayo iliipig KCB 1-0 Ijumaa ugani Sportpesa Arena Kaunti ya Murang’a.

Kwenye mechi nyingine ambazo zilichezwa jana Posta Rangers na Bidco United ziliagana sare tasa katika uga wa Kenyatta.

Matokeo sawa na hayo yalishuhudiwa kati ya Sofapaka na Kariobangi Sharks ugani Dandora.

Mbio za kuwania ubingwa wa KPL zinapoendelea kuwa ngumu, itabidi Bidco United (29), Murang’a Seal (29) na Nairobi City Stars (27) zipambane ili kusalia ligini msimu ujao.

Ingawa hivyo, timu ambazo zipo nafasi ya 11 hadi 15 pia bado hazipo salama zisipojizatiti kuwahi ushindi kwenye mechi nne zilizosalia msimu ukamilike.