Dimba

Shumah, Osoro na Madada waitwa kikosi cha CHAN

Na CECIL ODONGO July 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kenya imeanza maandalizi ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani (CHAN 2024) baada ya Kocha Benni McCarthy kutaja kikosi cha muda cha wanasoka 30 ambao wataingia kambini wiki hii.

CHAN itaandaliwa na Kenya pamoja na majirani wake Tanzania na Uganda kutoka Agosti 2 hadi Agosti 30.

Mvamizi wa Kakamega Homeboyz Moses Shumah ambaye alicheka na nyavu mara 17 kisha kutwaa Kiatu cha Dhahabu msimu uliokamilika anaongoza orodha ya waliotajwa katika safu ya mbele.

Mpinzani wake wa karibu Emmanuel Osoro wa FC Talanta na Ryan Ogam wa Tusker ambao walifunga mabao 16 na 17 mtawalia pia wametajwa kwenye kikosi hicho.

Huku Shumah na Osoro wakiwa walicheza karibu mechi zote kwa timu zao, Ogam hakuwa amecheza ligini tangu Februari kutokana na kuuguza jeraha.

McCarthy raia wa Afrika Kusini, pia amempa nafasi Mohamed Bajaber ambaye alishinda taji la KPL na Kenya Police.

Fowadi huyo alichangamkiwa na mashabiki kwenye sare ya 3-3 ambayo Kenya ilipata dhidi Gambia mnamo Machi 20 kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia mnamo 2026.

Bajaber aliyafunga mabao tisa kwenye msimu uliokamilika juzi na ni kati ya wanasoka chipukizi ambao wameonyesha talanta ya juu mno.

Katika safu ya kati amewadumisha Austin Odhiambo na Alpha Onyango huku kinda mahiri wa AFC Leopards Kelly Madada akipata nafasi pia kikosini.

Wachezaji wapya pekee ambao watakuwa wakichezea Stars kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho ni Keith Imbali wa Shabana pamoja na Yakeen Mutehali na Staphod Odhiambo, wote wanaosakatia Ulinzi Stars.

Kenya itaandaa mechi zake za Kundi A kwenye uwanja wa MISC Kasarani. Harambee Stars ipo katika kundi A na mabingwa wa 2018 na 2020 Morocco, Angola, mabingwa wa 2009 na 2016 Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kisha Zambia.

KIKOSI

MAKIPA.

Faruk Shikhalo (Bandari), Sebastian Wekesa (Kariobangi Sharks), Brian Opondo (Tusker FC)

MABEKI
Siraj Mohammed (Bandari FC), Manzur Suleiman (KCB), Pamba Swaleh (Bandari FC), Abud Omar (Kenya Police),Alphonce Omija (Gor Mahia), Sylvester Owino (Gor Mahia), Michael Kibwage (Tusker), Daniel Sakari (Kenya Police), Lewis Bandi (AFC Leopards), Kevin Okumu (KCB)

KIUNGO
Brian Musa( Kenya Police), Kelly Madada (AFC Leopards), Keith Imbali (Shabana), Alpha Onyango (Gor Mahia), Mathias Isogoli (KCB), Staphod Odhiambo (Ulinzi Stars), Austine Odhiambo (Gor Mahia), Ben Stanley (Gor Mahia)

FOWADI
Mohammed Bajaber (Kenya Police), Boniface Muchiri (Ulinzi Stars), David Sakwa (Bandari), Emmanuel Osoro (FC Talanta), Yakeen Muteheli (Ulinzi Stars), Edward Omondi (Sofapaka), Ryan Ogam (Tusker),Moses Shummah (Kakamega Homeboyz), Beja Nyamawi (Bandari).