Dimba

Team Kenya warejea nyumbani na kapu la dhahabu kutoka Dubai Grand Prix

Na GEOFFREY ANENE February 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TIMU ya Kenya imerejea Ijumaa usiku kutoka Milki za Kiarabu ambapo iliandikisha matokeo ya kuridhisha kwa kukamata nafasi ya tatu kati ya mataifa 52 yaliyoshiriki riadha za walemavu za Dubai World Para Atheltics Grand Prix jijini Dubai katika Milki za Kiarabu (UAE), kuanzia Februari 10-13.

India ilitwaa taji kwa medali 21 (dhahabu tisa, fedha nane na shaba nne) ikifuatiwa na Saudi Arabia (tisa, sita na nne), nayo Kenya (tisa, moja na sita) ikafunga mduara wa tatu-bora.

UAE (dhahabu nane, fedha sita na shaba saba), Uswisi (saba, moja na mbili), Uchina (tano, nne na moja), Ujerumani (nne, mbili na sifuri), Mauritius (tatu, sita na nne), Ukraine (tatu, tano na mbili) na Czech na Iran (tatu, nne na tatu) zilikamilisha 10-bora mtawalia.

Team Kenya wakiwasili katika uwanja wa JKIA jijini Nairobi mnamo Ijumaa usiku kutoka jijini Dubai. PICHA | HISANI

Barani Afrika, Kenya na Mauritius zilifuatana katika nafasi mbili za kwanza nazo Tunisia na Afrika Kusini zikafunga 20-bora duniani kwa dhahabu mbili, fedha mbili na shaba moja.

Walioshindia Kenya dhahabu ni mwanataekwondo, mchezaji wa badminton na mtimkaji Stency Neema (200m T47), Samwel Mushai (5000m na 1500m T11/12), Nancy Chelangat (400m T11 na 1500m T11/12, Jairus Okora (100m na 400m T13), Sheilla Wanyonyi (kurusha mkuki F12/13) na Brian Esogon (400m T12).

Wakenya wengine waliopata medali mjini Dubai ni John Lokedi (fedha 5000m T11/12 na shaba 1500m T11/12), Samson Ojuka (shaba kuruka umbali T36/37/38 na dhahabu 200m T37), Jackson Kpar (shaba 5000m T11/12), Jonathan Kyalo (shaba kuruka umbali T44), Rajab Chetty (shaba kurusha tufe F11/12/20) na Elijah Makini (shaba 100m T45/46).

Wanyonyi aliimarisha mtupo wake bora kwenye fani ya kurusha mkuki kutoka mita 30.69 hadi 35.03m.

Team Kenya iliyoshiriki makala hayo ya 16 ya michezo ya wazi maarufu Fazza Open:

Jairus Okora (100m T13 na 400m T13), Samson Ojuka (100m T37, 200m T37 na kuruka umbali T37), Jonathan Kyalo (100m T44 na kuruka umbali T44), Elijah Makini (100m T46 na kuruka umbali T46), Brian Esogon (400m T12), Jean Kipchumba (1500m T02 na 5000m T02), Samwel Mushai (1500m T11 na 5000m T11), Jackson Kpar (1500m T12 na 5000m T12) na John Lokedi (1500m T12 na 5000m T12).

Pia Evans Rutto (1500m T46), John Mueni (kupaisha baiskeli ya walemavu 1500m T54 na 5000m T54), Rajab Chetty (kurusha tufe F11), Stency Neema (100m T47 na 200m T47), Geoffrey Rotich (400m T02 na 1500m T02), Nancy Chelangat (400m T11 na 1500m T11), Sheilla Wanyonyi (kurusha mkuki F12) na Ann Wacuka (kurusha mkuki ukikalia baiskeli ya walemavu F55).