Usiku wa mahasidi Arsenal na Man Utd wakitiana makucha
ARSENAL wameshinda Manchester United mara tatu mfululizo katika mechi zilizopita – lakini hawajawahi kuwapiga mara nne mfululizo kulingana na historia ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Leo usiku, mahasimu hao wa tangu jadi wanakutana wakati Manchester United wamepoteza mechi saba kati ya tisa ugenini dhidi ya Wanabunduki, wakashinda moja na kula sare moja. Arsenal wanajivunia rekodi ya kutoshindwa na Mashetani hao Wekundu kwenye mechi sita zilizopita ugani Emirates.
Kwingineko, Chelsea watakuwa ugenini St Mary’s Stadium kucheza na Southampton, wakati Manchester City wakiwaalika Nottingham Forest ugani Etihad jijini Manchester.
Bruno Fernandes atakuwa kikosini
Ugani Emirates, kiungo Bruno Fernandes atakuwa kikosini baada ya kupata nafuu kutokana na jeraha dogo, huku Leny Yoro akitarajiwa kujumuishwa kikosini kwa mara ya kwanza tangu mwanzoni mwa msimu.
Kulikuwa na wasiwasi miongoni mwa mashabiki wa Manchester United baada ya Fernandes kuonekana akihimili machungu kwenye goti lake na kutumia barafu mwishoni mwa wiki baada ya kutolewa uwanjani katika kipindi cha pili katika mechi yao dhidi ya Everton ambayo walishinda kwa mabao 4-0 ugani Old Trafford.
Lakini sasa mashabiki hao ni wenye furaha tele baada ya kocha mpya, Ruben Amorim kutangaza kwamba raia huyo wa Ureno yuko fiti kucheza.
“Yuko tayari kucheza. Tumekutana na akanihakikishia kwamba yuko katika hali nzuri ya kucheza Jumatano usiku.”
Uwepo wa kiungo huyo ni nafuu kwa kikosi cha Manchester United baada ya kutatizika hapo awali kabla ya ujio wa Amorim ambaye ameandikisha ushindi mara tatu katika mashindano tofauti.
Leny Yoro aliyenunuliwa kwa Sh8.4 bilioni
Kadhalika, mashabiki wa United watakuwa makini kumtazama Yoro uwanjani kwa mara ya kwanza tangu anunuliwe kwa Sh8.4 bilioni akitokea Lille.
Yoro ambaye amekuwa akiuguza jeraha, hajachezea Manchester United mechi kubwa tangu aumie timu yake ilipokuwa nchini Amerika kwa mechi za maandalizi kabla ya msimu kuanza.
“Pengine Yoro atapata nafasi kikosini. Nimemuona katika mazoezi na kupata yuko fiti, kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuanza dhidi ya Arsenal, Jumatano.”
“Kwa hakika ana kipawa cha kipekee. Hajarejea kikamilifu kwenye mazoezi makali, lakini nimemuona akijiandaa na makundi madogo ya wachezaji kando ya uwanja mkuu. Ana kasi, ni mlinzi anayeweza kukabiliana vilivyo na washambuliaji wa aina yoyote, sina wasiwasi naye,” aliongeza.
Kwa mara nyingine, kocha Mikel Arteta atawategemea Bukayo Saka na Martin Odegaard ambao wamekuwa wakibeba Wanabunduki hao tangu msimu uanze.
Mikel Arteta: Tuna kikosi kizuri lakini sharti tujiandae vyema
“Tuko katika kiwango kizuri kwa sasa, lakini sharti timu ijiandae vyema badala ya kutegemea ubora wa kikosi,” alisema Arteta.
“Hii ligi ina upinzani mkali. Kumbuka tunacheza kila baada ya siku tatu.”
Ni mechi ambayo itabidi Saka acheze kwa makini baada ya kuonyeshwa kadi ya tatu ya njano Jumamosi wakicheza na West Ham United.
Kulingana na sheria za EPL, wachezaji wanaoonyeshwa kadi tano za njano ndani ya mechi 19 za kwanza wanapigwa marufuku ya mechi moja.
Katika mechi ya leo, United watacheza bila Lisandro Martinez na Kobbie Mainoo watakaoikosa mechi hiyo kutokana na kadi tano.
Kadhalika, kocha Amorim atapanga kikosi chake bila walinzi Victor Lindelof na Jonny Evans wanaouguza majeraha, hivyo, huenda nafasi zao zikajazwa na Harry Maguire, Matthijs de Ligt na Noussair Mazraoui.
Christian Eriksen na Mason Mount wako katika viwango vizuri vya kuimarisha safu ya kati, pamoja na Amad Diallo aliyeonyesha kiwango kizuri Jumapili dhidi ya Everton.
Wengine wanaotarajiwa kuwa kikosini ni Diogo Dalot, Marcus Rashford na Joshua Zirkzee.
Ratiba ya mechi za Jumatano, Desemba 4:
Southampton vs Chelsea (10:30pm), Manchester City vs Nottingham Forest (10:30pm), Newcastle United vs Liverpool (10:30pm), Everton vs Wolves (10:30pm), Arsenal vs Manchester United (11:15pm), Aston Villa vs Brentford (11:15pm)