Wanigeria wanuna baada ya Super Eagles kufungiwa Libya bila chakula wala kitanda
LAGOS, NIGERIA
SHIRIKISHO la Soka la Nigeria (NFF) limeitaka FIFA iadhibu vikali taifa la Libya kutokana na mapokezi duni dhidi ya Super Eagles ilipokuwa nchini humo kwa mechi ya marudiano ya AFCON 2025 iliyopangwa kuchezwa Jumanne.
Kwingineko, Cameroon imekuwa timu ya pili baada ya Burkina Faso kufuzu kwa fainali za AFCON 2025, baada ya kufikisha pointi 10 kutokana na ushindi wa 1-0 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya katika mechi ya Kundi J iliyochezewa Kampala, Uganda, Jumatatu.
Nchini Libya, kikosi cha Nigeria kilitarajiwa kutua mjini Benghazi, Jumapili lakini ndege yao ilielekezwa Al Abraq ambapo wachezaji walifungiwa katika uwanja wa ndege kwa zaidi ya saa 10.
Wachezaji hao walikwama uwanjani humo usiku kucha bila chakula wala malazi, mbali na kunyimwa mawasiliano, tukio lililosababisha kutochezwa kwa mechi hiyo iliyokuwa imepelekwa umbali wa kilomita 230, safari ya saa tatu unusu kutoka Tripoli kwa usafiri wa basi barabarani.
Afisa wa mawasiliano wa NFF amesema tayari wachezaji wamerejea nyumbani, huku NFF ikiandikia CAF barua rasmi ya kulalamika kuhusiana na hatua hiyo ya wachezaji kupewa mapokezi mabaya.
Ubalozi wa Nigeria nchini Libya ulishindwa kuingilia kati suala hilo kwa sababu ulihitaji kupata idhini kutoka kwa serikali ya Libya ambayo imegawanyika.
Nahodha wa kikosi hicho, William Troost-Ekong alisema kuwa walikataa kusafiri kwa basi kutokana na hali mbaya ya usalama nchini humo.
Zilipokutana katika mkondo wa kwanza mjini Uyo, Nigeria, wenyeji waliibuka na ushindi wa 1-0; bao lililofungwa na Fisayo Dele-Bashiru ugani Godswill Akpabio.
Licha ya kutocheza mechi hiyo ya marudiano, Nigeria wangali kileleni mwa Kundi D kwa pointi saba kutokana na mechi tatu huku Libya wakiwa mkiani kwa alama moja.
Waziri wa Michezo wa Nigeria, John Owan Enoh alisema kuwa serikali inajali mno maisha ya wachezaji, huku Shirikisho la Soka la Libya (LFF) likidai kutohusika katika njama zozote za kuvuruga usafiri wa timu ya Nigeria.
Taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imesema uchunguzi unakaribia kukamilika kuhusiana na tukio hilo la kuchukiza.
“Nimefanya mazungmzo na Rais wa CAF, Patrice Motsepe pamoja na Katibu wa shirikisho hilo, Veron Mosengo-Omba.
“Niliwaambia si tu kwa sababu ya kiwewe na matukio ya mateso ya kisaikolojia, bali kuna hofu ya usalama kutokana na mgawanyiko wa taifa hili linaloongozwa na makundi mawili tofauti kutokana na tofauti za kisiasa.”
Kuna madai kwamba wasimamizi wa soka nchini Libya walikuwa wakilipiza kisasi baada ya ndege yao kuelekezwa Port Hartcourt, huku wakilaumu Nigeria kwa kukosa kuwapa basi la kusafirisha wachezaji kwa safari ya kilomita 130 hadi Uyo kulikochezewa mechi ya mkondo wa kwanza.
Matokeo ya Jumatatu:
Burkina Faso 2 Burundi 0, Kenya 0 Cameroon 1, Gambia 1 Madagascar 0, Zimbabwe 3 Namibia 1, Togo 0 Algeria 1, Liberia 1 Equatorial Guinea 2, Eswatini 0 Msumbiji 3.