Dondoo

Balaa long’i ya lofa ikikwama kwa seng’eng’e akifuata uroda kwa mke wa jirani

Na JOHN MUSYOKI February 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAEWA, MASINGA

JOMBI wa hapa alijipata taabani alipofumaniwa na bawabu wa boma moja akiwa amekwama kwa ukuta baada ya long’i yake kunaswa na seng’eng’e.

Inaarifiwa kuwa  jombi huyo alikuwa na mazoea ya kumnyelemea mke wa jirani wakati mumewe yuko kazi jijini.

Jamaa aliamua kufululiza kwenda kumtembelea mwanadada huyo na alipofika langoni alimpigia simu ila haikujibiwa.

Akaamua kupanda ukuta aingie ndani ya boma lakini suruali yake ikanaswa na seng’eng’e na kukwama.

Kwa bahati mbaya bawabu alimfumania akidhani ni mwizi, lakini akapigwa na butwaa kupata ni mzee huyo.

“Kumbe ni wewe! Unataka nini katika boma hili usiku na wewe sio mwizi? Umekuwa mshirikina ama?” soja alimfokea huku majibwa yakibweka nusra yamtafune.

Mzee alipatwa na aibu kubwa huku mke wa mwenye boma akibaki kucheka tu alipoitwa kujionea kisanga.