Dondoo

Ajificha chooni kuhepa mademu

March 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na DENNIS SINYO

KHWISERO, KAKAMEGA

JOMBI mmoja alilazimika kujificha chooni baada ya mademu wawili kumsaka wakitaka hela za matumizi.

Inaarifiwa kwamba jamaa huyo alikuwa na mazoea ya kuwadanganya vipusa alikuwa akifanya kazi katika ofisi za kaunti ilhali hakuwa na kibarua chochote.

Fununu zinadai alikuwa na tabia ya kuwatumia wasichana na kisha kuwahepa akidai hakuwa tayari kuoa.

Inasemekana alikuwa akiahidi wasichana hao pesa kila mwezi jambo ambalo hangetimiza.

Wawili kati ya wasichana aliokuwa akidanganya walianza kumsaka awape pesa alizowaahidi.

Siku ya kioja, jamaa alikuwa ameketi nje ya duka moja akipiga gumzo na marafiki zake alipowaona wasichana hao wawili wakielekea alipokuwa.

Punde tu alipowaona, alipiga kona na kujificha kwenye choo katika kituo cha kuuza mafuta kilichokuwa karibu.

Vipusa hao walipomkosa walianza kufoka wakisema walitaka kumwaibisha hadharani ili akome kuwachezea kila mara.

“Akionekana hapa mwambieni tunazidi kumtafuta. Mwambieni akome huo ujanja wake la sivyo atajua sisi ni nani,” alifoka mmoja wa wasichana hao.

Kulingana na mdokezi, akina dada hao walipoondoka, jamaa alitoka chooni akitokwa na kijasho chembamba.

Marafiki zake walimshauri akome kuchezea wasichana wakidai alikuwa akijichafulia jina.

“Kama unataka kulinda jina lako, tafadhali wachana na hawa wasichana. Ikiwa uliwapa ahadi ya kuwatumia pesa, watumie kisha uachane nao,’’ alisema rafiki yake mmoja.

Inasemekana jamaa alijigamba kwamba yeye ni bingwa wa kuwaingiza mademu kwenye boksi na kisha kuwahepa kwani hakuwa tayari kuoa.

Marafiki zake walimweleza kwamba asipoacha tabia hiyo siku moja atakiona cha mtema kuni.

“Wanawake sio wa kuchezea, watakuweza siku moja,” walimwambia.

 

Azushia mkewe kupata mlango ukiwa wazi usiku

CHWELE, BUNGOMA

KALAMENI wa hapa, ambaye amekuwa akimchunga mkewe kama shilingi, alizua rabsha baada ya kupata mlango wa nyumba yao ukiwa wazi.

Kalameni huyo alijuana na mwanadada mmoja mrembo na wakaoana.

Urembo wa mwanadada huyo ulimfanya mumewe kushuku ana mipango ya kando na kuhofia anaweza kunyakuliwa na wanaume wengine.

Siku ya kisanga, kalameni alipitia kilabuni ili azime mwasho wa koo lake kwa mvinyo na usiku ulipoingia, alianza safari ya kuelekea nyumbani.

Kalameni alipigwa na butwaa kupata mlango wa nyumba ukiwa wazi.

“Sasa nimejua kwamba kuna mafisi wanaokuja hapa kunyemelea mali yangu na leo wamekuwa na tamaa wakasahau kufunga mlango,” jamaa alipayuka.

Inasemekana alijaribu kumrushia kofi lakini akahepa na kupiga nduru watoto wakaamka na kumpata jamaa kwenye sakafu.

Yasemekana mkewe alijifungia chumba cha kulala na kumuacha jamaa kulala. – Na KIMANI wa NJUGUNA

WAZO BONZO

Wazo Bonzo

Demu afokea jamaa wake kwa kugundua anaishi kibandani

SEGA, SIAYA

KIDOSHO mmoja wa hapa alimrushia mpenzi wake maneno makali baada kupata alikuwa amejenga nyumba ya msonge.

Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa akimwambia kipusa alikuwa amejenga nyumba nzuri na kila kitu kilikuwa sawa.

Kidosho alipigwa na butwaa alipopata kuwa jombi alikuwa amejenga nyumba matope iliyoezekwa nyasi.

Demu aliwaka na kuanza kumfokea jamaa vikali akimlaumu kwa kujengea kibanda.

“Mimi siwezi nikaishi kwenye kibanda. Muda huo wote umekuwa ukiniambia umejenga nyumba nzuri, sasa nionyeshe nyumba uliyokuwa ukidai,”demu alisema kwa hasira.

Jamaa kusikia hayo alijawa na wasiwasi na kumtuliza kipusa na kuahidi kumjengea nyumba nzuri baadaye. – Na MIRRIAM MUTUNGA

Mhubiri akasirika vyombo vya kanisa kutumiwa kwa densi

PASTA mmoja aliteta vikali vyombo vya kuhubiri kanisani vilipotumiwa kucheza nyimbo za densi.

Duru zasema mwanasiasa maarufu kutoka hapa alikuwa amekodisha vyombo vya kanisa la pasta kutumia katika mkutano uliokuwa umesubiriwa kwa hamu.

Yasemekana mkutano uliingia ndoa, DJ alipoangusha burudani la muziki, huku waliohudhuria wakibanjuka na kunengua viuno kwa raha zao.

Mchungaji alikosa utulivu moyoni na akaamuru ngoma izimwe mara moja, akisema vyombo vya kanisa sio vya kucheza muziki wa “kidunia.”

“Ama kweli barabara ya kwenda mbinguni ni nyembamba, hata sijui ni ibilisi gani alinituma kujumuika na wenye dhambi,” pasta alifoka na kuondoka akiahidi katu hatoruhusu vyombo vya kanisa kutumiwa kwenye mikutano ya kisiasa tena. – Na RICHARD MAOSI

Pokoyoyo