Machozi yamtiririka polo akinyenyekea mkewe asimteme
Na Nicholas Cheruiyot
Kaborok, Kericho
Kulikuwa na kioja katika mtaa huu jamaa alipompata mkewe akitoroka kurudi kwao na kumlilia asifanye hivyo.
Inaarifiwa kuwa polo aligombana na mkewe kuhusu masuala ya kinyumbani hivi majuzi.
“Jamaa alipochoshwa na maneno makali ya mkewe, alimsukuma hadi akaanguka chini kisha akatafuta amani kwa kuenda kutembea mtaani,” mdaku aliarifu.
Hata hivyo, baada ya muda mfupi alipigiwa simu na kaka yake kumfahamisha mkewe alikuwa amefunganya virago na kuondoka.
Mara moja jamaa aliomba pikipiki na kuendesha kwa kasi kwa kuelekea kwa wakwe zake.
Ilikuwa afueni alipopata mkewe njiani akibebwa na pikipiki. Alimuamrisha mwendeshaji kupiga breki naye akafanya hivyo haraka.
Huku akihema, jamaa alishika begi la mkewe na kumlilia asimtie aibu.
“Kwani ulikasirika sana nilipokugusa tu? Si ilikuwa mara yangu ya kwanza kunguruma kama simba? Naomba usinikosee heshima kwa wakwe wangu,” polo alilia machozi huku mkewe akiwa amenuna sana.
“Ulidhani unaweza kunitesa utakavyo na nigandie kwako kama gundi? Baba yangu bado ananipenda sana na kama hunitaki niache. Sirudi ng’o!” mrembo alisema na kutingisha kiuno kwa maringo.
Waendeshaji pikipiki walijiunga na mrengo wa polo na kumshauri mrembo arudi kwake.
“Nyinyi mnaheshimika katika kijiji hiki. Aibu iliyoje watu kusikia mlivurugana! Rudini kwenu na muongee hadi muelewane,” mwanabodaboda mmoja alishauri.
Hatimaye, mrembo alikubali kurudi akiwa ametoa masharti kuwa kamwe yeye si wa kuzushiwa.
“Nikiteleza nataka unieleze kosa langu polepole. Sina mazoea ya kupigiwa kelele na usipobadilika utajua hujui,” kipusa alisema na jamaa akaahidi kuzingatia hayo yote.