Dondoo

Mama afokea mkazamwana kwa kugeuza mumewe kuwa ‘mboch’

Na JANET KAVUNGA November 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAMA mmoja alizua kisanga katika nyumba ya mwanawe eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, akimlaumu mkaza mwana kwa kumgeuza mumewe kuwa kijakazi.

Mama anayeishi Mtopanga alifika kwa nyumba ya mwanawe kwa kishindo baada ya kudokezewa kuwa mkewe alikuwa amemkalia chapati huku akimlazimisha kufanya kazi za nyumbani.

“Mama alifika kwa kishindo na kumpata mwanawe akipiga deki. Alimzushia mkaza mwana kwa kumtumia vibaya mwanawe. Alikasirisha zaidi kwa kuwa demu alikuwa amemfukuza yaya aliyekuwa ameajiriwa na mumewe,” alisema mdokezi.

Mwanawe alipojaribu kuzungumza, mama alimzima kwa kumuuliza iwapo ni yeye aliyeoa au alikuwa ameolewa na mkewe.

Alimtaka mwanadada kumheshimu mumewe na kumpa haki zake kama mke la sivyo, amtimue.