Mhubiri ajuta kujenga kwenye ardhi ya umma
Na DENNIS SINYO
SHIBALE, MUMIAS
PASTA mmoja eneo hili, alililazimika kubadilisha kanisa kuwa chumba cha kulala baada ya nyumba yake ya kifahari kubomolewa kwa madai ilijengwa kwenye ardhi ya umma.
Inasemekana kwamba nyumba hiyo iliyogharimu mamilioni ya pesa ilikuwa imejengwa kwenye kipande cha ardhi ambacho kilikuwa kimetengwa kutumiwa na umma.
Kulingana na mdokezi, nyumba ilijengwa huku baadhi ya washiriki wa kanisa wakipinga na kumweleza pasta ardhi hiyo ilikuwa imenyakuliwa na matapeli.
“Pasta huyo aliwapasha habari washirika kwamba alikuwa ameona ploti iliyokuwa ikiuzwa na akawataka waumini kuchanga pesa kununua ardhi hiyo,” alisema mdokezi
Licha ya washiriki wengine kupinga, ardhi ilinunuliwa baada ya pasta kuwapuuza na ujenzi ukaendelea. “Maelfu ya pesa zilichangishwa kufanikisha ujenzi huo.Waumini kadhaa waliacha kwenda kanisani kwa kuhofia kuitishwa pesa za ujenzi.
Inasemekana ujenzi wa nyumba hiyo uligharimu zaidi ya Sh2 milioni.
Lakini hata kabla ya mwaka kuisha, notisi ilitolewa kwamba nyumba zote kwenye ardhi za umma zibomolewe katika muda wa miezi mitatu.
Mhubiri huyo hakuamini macho yake alipotazama kwa uchungu na masikitiko wakati tinga tinga lilipobomoa nyumba hiyo ya kifahari.
Baadhi ya washiriki waliokuwa wakipinga ujenzi huo, walianza kulaumu mhubiri kwa kupuuza maoni yao walipomshauri kuwa ploti hiyo ilikuwa imenyakuliwa.
Pasta alitokwa machozi na akalazimika kuhamia kanisani ambako amekuwa akilala na kufanyia shughuli zote.
Waumini wameapa kutochanga pesa zingine kugharimia ujenzi wa makazi mapya ya mhubiri huyo.
“Tulipinga ujenzi huo lakini tukapuuzwa. Sasa hatutatoa chochote kununua shamba au kujenga tena,’’ alisema muumini mmoja.