Dondoo

Polo atimuliwa ugenini usiku wa manane kwa kufunza watoto wa rafiki yake kubugia pombe

Na KIPNGENO CHERUIYOT November 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JOMBI mmoja alitimuliwa usiku na jamaa yake kwa kujaribu kuwaingiza watoto wa boma moja katika eneo la Kimulot, Kaunti ya Bomet, kwenye uraibu wa dozi.

Inasemekana jombi huyo ni mraibu sugu wa dozi licha ya hatua kadhaa kuchukuliwa na jamaa zake kumtoa kwenye shida hiyo.

“Juzi, jombi alifika kwa jamaa zake wanaoishi eneo hilo akiwa ameficha chupa kadhaa za dozi ndani ya begi lake,” mdaku akaarifu.

Mzee wa boma alipofika kwake usiku na kuarifiwa kuhusu uwepo wa mgeni huyo, alifululiza hadi katika nyumba wanakoishi wanawe wa kiume. Alimkuta mgeni akifurahia dozi huku akipiga gumzo na wanawe.

“Nimekuonya mara kadhaa usikaribie wanangu. Chukua kilicho chako na uondoke hapa mara moja. Wewe ni jamaa yangu lakini sipendi tabia zako,” buda alimfokea.

Baada ya dakika chache, polo alikuwa amemezwa na giza totoro na haikubainika alikoenda kulala.