Habari za Kaunti

Duale: Nitasafisha Mto Nairobi na kuzima kelele za matatu jijini

Na KEVIN CHERUIYOT August 13th, 2024 1 min read

WAZIRI mpya wa Mazingira Aden Duale ameapa kuwa atafuata nyayo za aliyekuwa waziri marehemu John Michuki kwa kutunza mito, misitu na kuhakikisha upanzi wa miti unaenziwa.

Bw Duale alisema kuwa anafahamu sheria zinazoongoza utunzaji wa mazingira na atatekeleza sheria hizo kikamilifu.

Chini ya uongozi wake, aliapa kuwa atatunza na kusafisha mto Nairobi ambao umeathirika kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Waziri huyo alikuwa akiongea Jumatatu, Agosti 12, 2024 katika Jumba la Mazingira ambako ni makao makuu ya wizara hiyo.

Alikuwa amekabidhiwa usimamizi wa wizara yenyewe na mtangulizi wake Soipan Tuya ambaye sasa ni Waziri wa Ulinzi.

Bw Duale alisema Nairobi huwa ni makao makuu ya Shirika la Kitaifa Kuhusu Mazingira (UNEP) na atakuwa akifanya kazi kwa karibu na Gavana Johnson Sakaja kurejeshea Nairobi hadhi yake ya zamani kama mji uliofahamika kuwa na madhari ya kijani kibichi.

Aidha, waziri huyo mpya aliwaonya wanyakuzi wa ardhi ya misitu na ile iliyo karibu na mito kuwa chuma chao ki motoni.

“Tutafuata sheria ambazo zimetungwa na kuwekewa raia. Huwezi kujenga au kushiriki kilimo katika ardhi iliyoko kando ya mto,” akaonya Bw Duale.

“Kama tunasafisha mto Nairobi basi ni lazima tuondoe majaa ya taka ambayo yapo karibu na mto huo,” akaongeza.

Aidha, aliahidi kupambana na uchafuzi wa mazingira kupitia kelele kutoka kwa matatu huku akiahidi kuwa kila matatu lazima itakuwa na jaa la taka.

Bw Duale ni mwanasiasa nguli ambaye amewahi kuhudumu kama mbunge wa Garissa Mjini (zamani Dujis), Kiongozi wa Wengi na pia sasa kama waziri.

Kabla Rais William Ruto kuvunja Baraza lake la Mawaziri Julai 2024 kufuatia presha ya Gen Z, Bw Duale alikuwa ameshikilia Wizara ya Ulinzi.

Alibahatika kurejea tena serikalini.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo