Maoni

Enyi wana bodaboda, tusijaribu nguvu za maji msimu huu wa mafuriko!

May 16th, 2024 1 min read

NA JURGEN NAMBEKA

HUKU mafuriko yakiendelea kushuhudiwa katika sehemu tofauti za nchi, visa vya Wakenya kadhaa kujiingiza katika hatari ya mafuriko vimewashtua wengi.

Mapema wiki hii, video moja ilisambaa mitandaoni ikionyesha mwendeshaji mmoja wa bodaboda akisombwa na maji ya mato uliofurika, kwa kudhani kuwa angeyashinda maji hayo nguvu na kuvuka hadi ng’ambo ya pili.

Cha kushangaza ni kuwa, licha ya yeye kuingia katika hatari hiyo mwenyewe, Wakenya kadhaa walikuwa kando ya mto huo, pamoja na ule aliyekuwa akinasa video hiyo.

Huenda mwendeshaji huyo angekuwa hai, iwapo tu waliokuwa hapo wangemwonya kuhusu kitendo chake.

Hiki siyo kisa cha pekee kwani kuna visa vingi vilivyoshuhudiwa katika msimu huu wa mvua za masika na hata wakati wa mvua za El Nino mwishoni mwa mwaka uliopita.

Ikikumbukwa vizuri, naibu Rais Rigathi Gachagua aliwahi kujipata kikaangoni baada ya kusema kuwa, baadhi ya Wakenya walioaga katika mafuriko, walijipeleka kwenye mauti wenyewe.

Kila uchao, naibu huyo aliwaonya Wakenya dhidi ya kuonyesha umahiri wao katika mito iliyofurika na kutaka kupita licha ya hali mbaya ya mito hiyo.

Kwa mwendeshaji wa pikipiki aliyesombwa na maji, ni wazi kuwa wosia wa Bw Rigathi uliangukia sikio la kufa ambalo kwa kawaida halisikii dawa.

Ni ombi langu kuwa, licha ya kuwa mara nyingine watu huweza kukwepa hatari kwa kuwa maji hayana nguvu, kuna sehemu ambazo kwa kupima tu na macho, ni vyema kukaa kando hadi msaada upatikane au maji yapungue.

Ni vyema tuwaonye raia wenzetu ma hasa wanabodabora wanaojipeleka katika hatari kwa kudai kuwa wao wana uwezo wa kukabiliana na mafuriko.