Habari Mseto

Familia 30 zaachwa bila makao nyumba zao zikibomolewa usiku

Na STANLEY NGOTHO  September 6th, 2024 1 min read

FAMILIA zaidi ya 30 zilibaki bila makazi baada ya nyumba zao kubomolewa Ijumaa asubuhi, Septemba 6, 2024 eneo la Kwa Munyeti, Kaunti Ndogo ya Athi River, Machakos kutokana na mzozo wa shamba.

Kulingana na waathiriwa hao, watu wasiojulikana na ambao walivalia sare rasmi za polisi, walivamia eneo hilo saa kumi alfajiri.

Waliamrishwa kutoka nje ya makao yao, kabla ya nyumba zao kubomolewa kwa matingatinga.

Wakati wa vurugu zilizofuatia, watu wawili waliopata majeraha walikimbizwa hospitalini kupata matibabu.

Bw Peter Kasyoki aliyeishi kwa shamba hilo kwa miaka miwili baada ya kulinunua, alisema hawakuwa na notisi ya kuhamishwa wala amri ya mahakama.

Hali hiyo, iliwaacha wakihesabu hasara ya mamilioni ya pesa bila msaada wowote.

Bw Said Masase Mochama, alikemea tukio hilo, akisema watu hao walikosa kujitambulisha. Walipowauliza, waliwatishia.

“Kulikuwa na polisi wengi. Waliondoka baada ya nyumba zetu kubomolewa. Nilikuwa nimechukua mkopo ili kujenga. Nina huzuni. Hii sio njia ya ustaarabu kutatua mzozo wa umiliki wa ardhi,” alisema Bw Mochama.

Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Athi River Mashariki Bi Mary Njoki hakupatikana kutoa maoni.