• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Kaburi la bahati nzuri lavutia watalii kutoka pembe zote za dunia

Kaburi la bahati nzuri lavutia watalii kutoka pembe zote za dunia

NA KALUME KAZUNGU

JINA la Mwanahadie Famau linatambuliwa na wengi, hasa katika jamii ya Waswahili Wabajuni wa asili ya Lamu.

Ni mwanamke ambaye kaburi lake ndilo linalotambuliwa kuwa la jadi zaidi kisiwani Lamu kwa mujibu wa Halmashauri ya Makavazi na Turathi za Kitaifa nchini (NMK).

Likipatikana mtaa wa Mkomani kisiwani Lamu, kaburi hilo linaaminika kudumu kwa zaidi ya miaka 400 kwa sasa.

Jina kamili au asilia la Bi Mwanahadie Famau ni ‘Mwanadia Wa Mbwarafamau Wa Shee.’

Ni mzawa wa mtaa wa Uwani, kijiji cha Mvundeni, lokesheni ya Mkokoni iliyoko tarafa ya Kiunga, Lamu Mashariki.

Ni mwanamke aliyefahamika sana kwa jinsi alivyokuwa tajiri miongoni mwa Wabajuni.

Pia anatambulika kwa alivyomcha Mungu (Allah).

Bi Famau mara nyingi alijitenga kabisa na mambo ya kilimwengu, hali inayomfanya hadi leo kuheshimiwa na kuchukuliwa na wengi kuwa mtawa wa Lamu.

Hakuolewa kwani dhihirisho hilo linatokana na kwamba hakuacha mwana hata mmoja.

Licha ya hayo, aliishi akiheshimu dini na jamii kwa kiasi kikubwa.

Alikuwa mwingi wa upendo, akijitolea kuwasaidia wasiojiweza na kupigania haki za jamii ya Wabajuni.

Bi Famau anajulikana kwa jinsi alivyotumia utajiri wake kufadhili vita vya kuikomboa jamii ya Wabajuni kutoka kwa minyororo ya maadui, hasa Wagalla.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Afisa Msimamizi wa Makavazi na Turathi za Kitaifa, tawi la Lamu katika NMK, Bw Mohammed Ali Mwenje alisema hulka ya Bi Famau ya kumcha Mungu na kuenenda sawasawa na maadili ya dini na jamii imesukuma waja, ikiwemo wenyeji, wageni na watalii kuzuru kaburi lake kila mara, wengine wakitekeleza dua ya kujitakia mema maishani.

Aghalabu kaburi la Bi Mwanahadie Famau linachukuliwa kuwa kaburi la bahati nzuri, kigezo ambacho kimevutia wenyeji, wageni na watalii kutoka pembe zote za dunia.

“Kama NMK, tunaamini kaburi la Bi Mwanahadie Famau ndilo la zamani zaidi lililoko eneo hili la Lamu. Tunalikadiria kudumu kwa zaidi ya miaka 400. NMK imeliorodhesha kaburi hilo miongoni mwa makavazi na tunalitunza. Bi Mwanahadie Famau anachukuliwa kama mtawa kutokana na jinsi alivyoishi akifuata mienendo ya dini ya Kiislamu na kuheshimu jamii yake. Miaka 400 tangu kifo chake, kaburi lake limegeuzwa kuwa kiungo muhimu cha historia. Watu hutoka mbali na karibu kuja kujionea kaburi hili la kipekee. Kuna wengine hata hufanya maombi katika kaburi la Bi Famau, wakiamini watajiletea mema au bahati njema maishani,” akasema Bw Mwenje.

Mwanahistoria na Mzee wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana Shee anamtaja Bi Mwanahadie Famau kuwa mwanamke wa haiba kubwa na wa kuheshimika eneo hilo licha ya kufariki miaka mingi iliyopita.

Anasema jamii ya Lamu, hasa Wabajuni wanamuenzi vilivyo Bi Famau, wakijua fika juhudi zake katika kuitetea jamii ya Wabajuni zilichangia pakubwa maendeleo ya jamii hiyo na eneo zima la Lamu kwa ujumla.

Bw Mbwana anasema utiifu wa Bi Famau, hasa kuhusiana na masuala ya dini pia ulichochewa na jinsi wazazi wake walivyotambulika kuwa wanavyuo wakuu miongoni mwa jamii ya Wabajuni.

“Familia ya Bi Famau twaichukulia kuwa kitovu cha jamii ya Wabajuni wa leo walioko Lamu. Nduguye Bi Famau alijulikana kama Bw Lali Wa Shee Mbwarafamau. Yeye ndiye aliyeongoza mapigano dhidi ya Wagalla waliokuwa wakidhulumu Wabajuni eneo letu la Mvundeni, tarafa ya Kiunga. Familia ya Bw Mbwaraframau ndiyo iliyopanuka na kupata Wabajuni wa leo eneo hili,” akasema Bw Mbwana.

Kulingana na Bw Mbwana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, utajiri wa Bi Famau ulitokana na jinsi alivyoibukia kilimo kwa wingi, akikuza mahindi, mawele, wimbi, mtama nakadhalika.

Bi Famau pia alikuwa mwanabiashara tajika enzi zake.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa na Taifa Leo waliiomba serikali kupitia kwa NMK kuhakikisha makaburi ya zamani, ikiwemo lile kongwe zaidi la Bi Mwanahadie Famau yanapewa ulinzi maalumu.

Mbali na kaburi la miaka 400 la Bi Mwanahadie Famau, mengine ni lile la Liwali wa zamani wa Lamu, Bw Zahid Ngumi na mkewe, yote yakipatikana mtaa wa Langoni kwenye mji wa Kale wa Lamu.

Makaburi hayo yamedumu kwa zaidi ya miaka 200 eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa mbali na kuwa mtawala, Zahidi Ngumi pia ndiye mhandisi mkuu aliyeongoza ujenzi wa  jumba la Lamu Fort  kati ya mwaka 1813 hadi 1821.

“Makaburi ya watu wetu wa zamani kama Bi Mwanahadie Famau na liwali, Zahid Ngumi na wengineo yanafaa kuzingirwa seng’enge. Wengi wamekuwa wakitupa taka ovyo kwenye maeneo ambapo makaburi ya jadi hupatikana na hairidhishi kamwe,” akasema Bi Fatma Alwy, mkazi wa kisiwa cha Lamu. 

  • Tags

You can share this post!

Mashujaa Dei: Hoteli za Kericho na kaunti jirani zavuna...

Ezra Chiloba ajiuzulu kutoka wadhifa wake wa Mkurugenzi...

T L