Habari za Kitaifa

Gachagua azidi kulilia umoja wa Mlima Kenya

Na STANLEY NGOTHO August 25th, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesisitiza kuwa vitisho havitazuia juhudi zake za kuunganisha eneo pana la Mlima Kenya.

Akizungumza katika eneo la Inkinyie – Dalalekutuk, Kaunti Ndogo ya Kajiado ya Kati, Naibu Rais alisema hataogopa kuunganisha eneo la Mlima Kenya.

Alilaumu wanasiasa wa eneo hilo – bila kuwatambua – ambao wamekuwa wakipinga wito wake akiwataja kama waoga ambao hupata tu ujasiri wanapozungumza katika majukwaa ya mitandao ya kijamii.

“Mimi si mwendawazimu kuomba eneo la Mlima Kenya kuungana. Tunaenda kuunganisha Wakenya lakini tutawaunganisha kuanzia jamii,’ alisema Bw Gachagua.

Aliongeza: “Kenya ni taifa la jamii ambazo lazima ziheshimiwe ili kufikia utangamano wa kitaifa. Baada ya kila jamii kuungana baina yao kitakachofuata ni jamii zote kuungana kwa pamoja kuunda taifa imara.”

Bw Gachagua alihimiza jamii ya Maasai iungane na kutokubali kuyumbishwa na migawanyiko ya kisiasa.

Alihimiza jamii hiyo kushirikiana na wenzao wa Mlima Kenya kijamii, kibiashara na kisiasa.

“Umuhimu wa jamii ya Maa katika mazungumzo ya kisiasa ya Kitaifa hauwezi kupuuzwa. Heshima kwa jamii kuketi katika meza ya maamuzi ya Kitaifa hutokana na umoja,’ Bw Gachagua alisema na kuwakashifu baadhi ya mabroka wa kisiasa wanaodaiwa kuwazuia viongozi wa Kajiado kumfikia Rais William Ruto.

Alimshukuru Rais kwa kuzungumza na wapinzani wake wa kisiasa ili kutuliza nchi.

“Ninamshukuru Rais Ruto kwa kufungua milango kwa Wakenya kuzungumza licha ya misimamo yao ya kisiasa. Tunatafuta marafiki wapya katika nchi nzima ili kuwa na taifa dhabiti,’ aliongeza.

Mkutano wa Mwaka wa Umoja wa Maa, huleta pamoja jamii zinazozungumza Maa kwa maombi kila mwaka.

Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, ambaye pia ni msemaji wa jamii za Maa, alihimiza utawala wa Kenya Kwanza kubuni mbinu za kushughulikia masuala yanayoathiri kaunti ziliko jamii za Maa.

‘Kaunti za Maa zinaunga serikali ya Kenya Kwanza lakini tunataka mfumo wa jinsi ya kushughulikia masuala yetu. Haikunipendeza wakati Rais alipotangaza ujenzi wa barabara ya Ilasti-Taita Taveta na kuhusu Hifadhi ya Kitaifa ya Amboseli lakini mtumishi wa umma baadaye akadai vinginevyo, ‘alisema Gavana Lenku.

Wengine walioandamana na Naibu Rais ni pamoja na Naibu Gavana Martine Moshisho, Seneta wa Kajiado Samuel Seki, Samuel Parashina (Mbunge wa Kajiado Kusini), Onesmus Ngogoyo (Mbunge wa Kajiado Kaskazini) na Seneta Mteule Peris Tobiko miongoni mwa wengine.

Baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wamekuwa wakikosoa wito wa Gachagua wa kuunganisha eneo hilo wakisema analitenga na utawala wa Rais William Ruto.

Mbunge wa Laikipia Mashariki, Bw Mwangi Kiunjuri amesisitiza kuwa wito wa Bw Gachagua hauna nia njema na kuapa kupinga juhudi zake.