Habari za Kitaifa

Gachagua: Raila ni kiboko yao Afrika

Na BENSON MATHEKA August 27th, 2024 1 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amemmiminia sifa kiongozi wa upinzani Raila Odinga akisema anafaa kwa wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa (Afrika AUC).

Ni kutokana na jitihada za Bw Odinga kupigania demokrasia na maendeleo ya Kenya, ambapo Nabu Rais Gachagua ameelezea imani yake kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani anafaa pakubwa kuongoza muungano huo wa kibara.

“Huu ni wakati muhimu kwa nchi yetu. Tunazindua kiongozi bora zaidi wa Kenya kuongoza Afrika. Watu wa Kenya wameungana nyuma ya Raila awe mwenyekiti wa AUC. Afrika, bara letu, linahitaji kiongozi bora zaidi,” Bw Gachagua alisema.

Alisema hayo Jumanne, Agosti 27, 2024 wakati wa uzinduzi rasmi wa Bw Raila kama mgombea wa uenyekiti AUC kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Rais William Ruto na kuhudhuriwa na marais na viongozi kadha kutoka Afrika Mashariki, ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi.

Bw Gachagua alisema kwamba uhasama wake wa awali na Bw Odinga ulikuwa wa kisiasa.

“Watu wanaweza kushang’aa kwa nini ninamsifu Raila ilhali nilisema mambo tofauti kumhusu awali. Sina ubaya wa kibinafsi na Raila. Ni kwa kuwa alikuwa akishindana na mkubwa wangu wakati wa kampeni,” Gachagua alisema.

Alisema ana hakika Afrika itastawi chini ya uongozi wa Raila iwapo atachaguliwa kuongoza Tume ya Muungano wa Afrika.

“Kama mtu msema ukweli na anayesikiliza mashinani watu wanavyosema, ninahakikisha kuwa Wakenya wote wako nyuma ya Raila kwa wadhifa wa AUC,” alisema Bw Gachagua.