Habari MsetoSiasa

Gavana Wa Iria afichua sababu za kususia vikao

February 27th, 2020 1 min read

Na NDUNG’U GACHANE

GAVANA wa Murang’a, Bw Mwangi wa Iria ameelezea sababu yake ya kukosa kuhudhuria vikao vitatu vya kujadili maandalizi ya mkutano wa Mpango wa Maridhiano (BBI) utakaofanyika kesho katika Kaunti ya Meru.

Gavana wa Iria hakuwepo wakati magavana wa Mlima Kenya walipokutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika afisi yake kwenye jengo la Capitol Hill.

Magavana Waiguru, Bw Kiraitu Murungi (Meru), Muthomi Njuki (Tharaka-Nithi), Francis Kimemia (Nyandarua), Murithi Ndiritu (Laikipia) na Martin Wambora (Embu) walihudhuria kikao hicho.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Wa Iria alisema alikosa vikao hivyo kwa sababu alikuwa akikusanya maoni kutoka kwa wakazi wa Murang’a.

“Murang’a ndiyo kaunti ya pekee ambayo imeandaa mkutano wa hadhara kuwezesha wakazi kutoa maoni yao kuhusiana na BBI. Jumla ya watu 10,000 walijitokeza kutoa maoni yao,” akasema Bw wa Iria na kuongeza kuwa viongozi hawafai kujifungia hotelini kujadili ripoti ya BBI.

“Wakati wa uzinduzi wa ripoti ya BBI katika ukumbi wa Bomas, Rais Kenyatta alisema hiyo ilikuwa zamu ya Wakenya kupekua ripoti hiyo na kutoa maoni yao.

“Lakini hatuwezi kujadili tipoti hotelini. Mikutano ya kujadili ripoti inafaa kufanyika hadharani ili kila mwananchi ashiriki,” akasema.

“Mkutano uliofanyika katika hoteli ya Thika Greens ulikuwa na ubaguzi kwani baadhi ya watu hawakutakiwa,” akaongezea.