Habari za Kitaifa

Gen Z wa North Rift wakata keki kukejeli aliyekuwa waziri wa barabara Murkomen

Na TITUS OMINDE July 14th, 2024 2 min read

KUMWAGA unga kwa aliyekuwa waziri wa barabara Kipchumba Murkomen kumekuwa sherehe kwa baadhi ya vijana almaarufu Gen Z kutoka North Rift, ngome ya waziri huyo.

Ilikuwa kinaya wakati baadhi ya vijana hao walipofanya sherehe ya kukata keki kushukuru Rais William Ruto kwa kumwachisha kazi waziri Murkomen pamoja na mawaziri wote 22 ambao waliachishwa kazi kutokana na shinikizo za vijana wa Gen Z kama baadhi ya mabadiliko muhimu ambayo walitaka rais kuyatekeleza.

Wakati wa sherehe hiyo ya kukata keti iliyofanyika mjini Eldoret karibu na jengo ambalo linadaiwa kumilikiwa na Bw Murkomen, vijana hao walitamka maneno kwa lugha ya Kikalenjin ambayo yalionekana kama tambiko ya kulaani hatua yeyote ya kumrudisha Murkomen kazini hasa katika baraza la mawaziri.

Keki ya ‘kusherehekea’ kufutwa kazi kwa aliyekuwa Waziri Kipchumba Murkomen, North Rift. Picha|Titus Ominde

Wakiongozwa na rais wa vuguvugu la vijana North Rift Kelvin Kipleting, walishukuru rais kwa hatua hiyo huku wakitaka wembe huo uendelezwe hadi kwa makatibu wakuu ambao wamezembea katika wizara zao.

“Murkomen amekuwa na tabia ya kutudharau na kutukejeli sisi kama vijana leo hii tunakata keki ya kusherehekea uamuzi wa busara wa rais huku tukimkaribisha kujiunga na kundi la vijana wasiokuwa na kazi ili hata yeye ahisi vile tumemkuwa tukisikia wakati alikuwa akituonyesha madharau na kutojali,” alisema Kipleting.

Naye Humphrey Omondi ambaye ni mwakilishi wa kundi la muungano wa chipukizi maarufu Gen Z without Boundaries mjini Eldoret alisema masaibu ya rais William Ruto yamechangiwa pakubwa na mawaziri wenye kiburi kama Murkomen miongoni mwa wengine wengi.

Kwa sasa wanataka wale ambao watateuliwa kuwa mawawizri wateuliwe kwa muujibu wa taaluma ambazo wamesomea.

“Kila wizara yapaswa kuongozwa na mtaalam wa sekta husika kwa mfano elimu awe msomi wa elimu, kilimo awe msomi wa masuala ya kilimo na kadhalika,” aliongeza Bw Omondi

Vijana hao pia walitaka rais kufanyia mabadiliko kamati za bunge huku wakitaka nafasi ya kiongozi wa wengi bungeni kuondolewa kwa Kimani Ichungwa kwa kumtaja kuwa kiongozi mwingine mwenye kiburi ambaye hajali maslahi ya Wakenya wengine.

“Tunasubiri kuona uongozi wa bunge ukiiga mfano wa rais kwa kuvunjilia mbali kamati zote za bunge na kuchagua viongozi wapya. Hatutaki viongozi kama Kimani Ichungwa na Silvanos Osoro wawili hao ni fedheha kwa vijana na bunge la Kenya kwa jumla aliongeza Bw Omondi.