Habari za Kitaifa

Gen Z walisababisha hasara ya Sh94 milioni walipovamia Bunge

Na MARY WANGARI July 23rd, 2024 2 min read

BUNGE la Kitaifa linakadiria hasara ya Sh94 milioni kufuatia maandamano ya kulalamikia Mswada wa Fedha 2024 ambapo Gen Z walivamia na kuteketeza kijisehemu cha Bunge mwezi uliopita, Juni 25.

Haya ni kwa mujibu wa Spika la Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula, akihutubia vyombo vya habari jana, Jumatatu, Julai 22, 2024 ambapo alisema kuwa shughuli ya ukarabati imekuwa ikiendelea tangu wabunge walipokwenda kwenye likizo fupi wiki tatu zilizopita.

Wabunge watarejelea vikao vyao hii leo, Jumanne, Julai 23, 2024 huku Spika Wetangula ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) akisema kuwa, “tunamshukuru Mungu hakuna mbunge au mfanyakazi wa bunge aliyeuawa katika tukio hilo.”

“Bunge la Kitaifa litarejelea shughuli zake kesho (Jumanne) huku likisubiriwa na ajenda kadhaa muhimu baada ya tukio la kusikitisha lililoshuhudiwa Juni 25. Tunawahakikishia Wakenya, kama Bunge, kuwa tumejitolea kuona kuwa sheria tunazopitisha ni bora kwa taifa letu,” alisema Bw Wetangula.

Kuhusu Mswada wa Fedha 2024, uliofutiliwa mbali, Spika Wetangula alisema Bunge litaangazia notisi iliyotumwa na Rais William Ruto akipendekeza vipengee vyote 69 vya mswada huo kufutiliwa mbali, akisema tayari amewasilisha notisi hiyo kwa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha.

“Spika anapaswa kutuma notisi kwa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipangilio ya Kitaifa baada ya kuipokea kutoka kwa Rais. Nilituma notisi hiyo kwa Kamati ili iangaziwe na ripoti iwasilishwe bungeni.”

Alisema hatua ya Rais kufutilia mbali vipengee vyote vya Mswada huo ilitokana na haja ya kusikiza kilio cha Wakenya waliokataa kabisa mswada huo.

Aidha, alifafanua kwamba Bunge, baada ya kupokea orodha ya mwisho, litawapiga msasa mawaziri wote ikiwemo waliorejeshwa baada ya kufutwa kazi kwa sababu itachukuliwa kama uteuzi mpya.

Kando na mchakato wa kufanyia mageuzi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wabunge pia wanasubiriwa na kibarua cha kuangazia miswada kadhaa ikiwemo kuhusu Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), Mswada wa Kufanyia Marekebisho Sheria kuhusu Barabara, Mswada wa Sukari na Sheria.

Bw Wetangula pia alifafanua ripoti kuhusu vyombo vya habari kuzuiwa kuangazia shughuli za Bunge la Kitaifa akisema hakuna kituo kilichozuiwa.

Alisema masharti fulani yamewekwa kufuatia uharibifu uliosababishwa na waandamanaji huku shughuli za ukarabati zikiendelea na kufichua kuhusu mpango wa kujenga kituo kipya cha wanahabari ndani ya majengo ya bunge.

“Nataka kufafanua kwamaba hakuna shirika la habari limezuiwa kuangazia Bunge. Tuna kisa kimoja tu kuhusu mwanahabari anayeshutumiwa kwa kukiuka kanuni za kimaadili na ambaye anachunguzwa na asasi za kiserikali, na ameagizwa kukakaa kando,” alisema.