Makala

Gharama ya juu ya mahari yachachisha wizi wa mifugo

Na DAVID MWERE September 10th, 2024 1 min read

UCHUNGUZI wa kina uliofanywa na wabunge umefichua jinsi gharama ghali ya mahari na mtindo wa wanasiasa kuwapa silaha majambazi ndizo chanzo cha ujangili na ukosefu wa usalama katika kaunti sita za Kaskazini Mashariki.

Hali ya usalama katika kaunti za Baringo, Elgeyo Marakwet, Turkana, West Pokot, Samburu na Laikipia, imeathiriwa na shughuli za uhalifu kutokana na ujangili, wizi wa mifugo na mapigano ya kiukoo.

Huku idadi kubwa ya wahasiriwa wakiwa wanawake, watoto na wazee, ukosefu wa usalama eneo hilo umesababisha vifo, wanajamii wasio na hatia kufurushwa makwao na misukosuko ya kiuchumi.

Uchunguzi wa wabunge uliochukua muda wa miezi tsa kutoka Agosti 2023 hadi Aprili 2024, umeonyesha kuwa ujangili na wizi wa mifugo hutokana na masuala kadhaa.

Masuala haya ni pamoja na biashara ya mifugo wa kuibwa, thamani inayotwikwa mifugo, itikadi za kitamaduni, matumizi ya mifugo kama malipo ya mahari eneo hilo ikiwemo haja ya kufidia baada ya kipindi kirefu cha kiangazi.

“Kero la ukosefu wa usalama eneo hili linatokana na itikadi zilizopitwa na wakati kama vile uvamizi wa mifugo unaoshinikizwa na malengo ya kibiashara, malipo ghali ya mahari, kujaza pengo baada ya vipindi virefu vya kiangazi na sifa wanazotwikwa vijana mashujaa vitani,” inaeleza ripoti iliyowasilishwa na Kamati inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi, Gabriel Tongoyo.

Isitoshe, ripoti hiyo inaashiria changamoto wanazopitia wanaume wanaotaka kuoa huku wakihitajika kukusanya mahari inayolipwa kwa kutumia mifugo kabla ya kupatiwa wake.

“Wanaume vijana wanaotaka kuoa wanashinikizwa na kulazimika kutumia kila wawezalo kupata mifugo wa kutimiza wajibu huo wa kijamii. Suala hili linavuruga hali ya usalama eneo hilo,” ilisema ripoti.

Aidha, kuna “mtindo wa kutatiza” ambapo wizi wa mifugo umegeuzwa kuwa biashara.

Mifugo walioibwa sasa wanauzwa kwa mapato ya kifedha badala ya malengo ya kitamaduni ya kuongeza mifugo.

Mabadiliko haya kutoka sababu za kitamaduni hadi faida ya kifedha yamechochea athari hasi za visa hivi na madhara yake kwa jamii.