Mpango wa upangaji uzazi wazinduliwa Lamu
NA KALUME KAZUNGU
IDARA ya Afya Kaunti ya Lamu imezindua rasmi mpango maalum utakaotumika katika utekelezaji wa shughuli za upangaji uzazi eneo hilo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Mpangilio huo unaokadiriwa kugharimu serikali ya kaunti ya Lamu kima cha Sh 136 milioni utatumika kati ya mwaka 2018 hadi 2020.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpangilio huo iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Mwana Arafa mjini Lamu Ijumaa, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afya eneo hilo, Dkt David Mulewa, alisema azma kuu ya kuzinduliwa kwa mpangilio huo ni kuinua kiwango cha matumizi ya mbinu za kupanga uzazi kote Lamu.
Idadi ya wakazi wanaotumia mbinu za kupanga uzazi kaunti ya Lamu bado iko chini, ambapo ni asilimia 43 pekee ya wakazi ndio wanaotumia mbinu mbalimbali zilizoko za kupanga uzazi.
Dkt Mulewa alisema wanalenga kuinua kiwango cha wanaopanga uzazi eneo hilo kutoka asilimia 43 hadi angalau asilimia 46 kufikia 2020.
“Tunafuraha kwamba leo tuko hapa kuzindua mpangilio maalum utakaosaidia kuhimiza wakazi kupanga uzazi. Mpango huu utatumika kuanzia mwaka huu wa 2018 hadi mwaka 2020. Furaha yetu ni kuona idadi ya wanaotumia mbinu za kupanga uzazi eneo hili inaongezeka kutoka asilimia 43 hadi asilimia 46 kufikia mwaka 2020. Ningewasihi wakazi kuibukia mbinu za kupanga uzazi kwa manufaa yao,” akasema Dkt Mulewa.
Naye Afisa Mkuu wa Idara ya Huduma za Matibabu, Kaunti ya Lamu, Dkt Abubakar Badawi, aliwahimiza wakazi kuukubali mpangilio huo na kukumbatia mbinu za upoangaji uzazi kwa manufaa yao.
Dkt Badawi alisema ni kupitia mbinu za upangaji uzazi ambapo vifo vya akina mama wajawazito na watoto ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa eneo hilo vitapungua.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Kaunti ya Lamu, Bi Anne Gathoni, aliutaja uzinduzi wa mpango huwa kuja kwa wakati ufaao.
Bi Gathoni aliwahimiza wanaume kuwaunga mkono wake zao katika shughuli nzima ya upanmgaji uzazi.
“Kuna baadhi ya wanaume ambao bado wako na dhana kwamba kupanga uzazi ni jukumu la wanawake pekee. Huo ni uongo. Ni jukumu lenu pia nyinyi wanaume kujitolea na kuwaunga mkono akina mama ili kufaulisha shughuli nzima ya upangaji uzazi kwa manufaa yetu sote,” akasema Bi Gathoni.
Naye Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri ambaye alihudhuria uzinduzi wa mpangilio huo wa Kaunti aliwataka wakazi kujitolea kwa kila hali ili kufaulisha mpango wa upangaji uzazi.
Aliwashauri wakazi kupanga uzazi ili kuwa na familia wanazoweza kuzikimu.