Habari Mseto

2019: Kamatakamata ya kila Ijumaa ilitesa mafisadi

December 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

Mwaka huu hautasahaulika hasa miongoni mwa maafisa wengi wakuu serikalini wakiwemo mawaziri, makatibu wa wizara mbalimbali, magavana, wanasiasa na watumishi wa umma.

Ulikuwa mwaka ambao wengi wa maafisa hao walitiwa nguvuni siku za Ijumaa na kuzuiliwa wikendi yote hadi Jumatatu waliposhtakiwa kwa madai ya ufisadi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji aliamuru washtakiwe baada ya tume ya kupambana na ufisadi (EACC) kukamilisha uchunguzi dhidi yao.

EACC ilipeleka kwa DPP majina ya washukiwa waliokuwa wameshachunguzwa.

DPP naye alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) wawatie nguvuni.

Wengi wa washukiwa hawa walitiwa nguvuni Ijumaa na kuzuiliwa katika vituo vya polisi wikendi nzima kabla ya kufikishwa kortini Jumatatu iliyofuatia.

Baadhi ya waliokamatwa ni Waziri wa Hazina Kuu ya Kitaifa Henry Rotich na katibu wake Kamau Thugge.

Rotich, Thugge pamoja na vinara wa Mamlaka ya ustawishaji bonde la Kerio (KDVA) walifunguliwa mashtaka ya ufujaji pesa za ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Aror.

EACC ilidai zaidi ya Sh20 bilioni zilifujwa zilipolipwa mkandarasi kutoka Italia.

Mabwawa haya mawili yalipelekea Serikali kupoteza zaidi ya Sh63bn na kufikia mwaka utamatike hakuna hata ujenzi uliokuwa umeanza.

Kashfa hii ya mabwawa haya ilichafulia Serikali ya Jubilee ambayo haikuwa makini kulinda pesa za walipa ushuru, jina.

Mbali na Rotich, Magavana Ferdinand Waititu ‘Baba Yao’ (Kiambu), Mike Sonko (Nairobi), Moses Kasaine Lenolkulal (Samburu) na Sospeter Ojaamong (Busia) walishtakiwa kwa ufujaji pesa za kaunti.

Waititu anadaiwa alifuja zaidi ya Sh580 milioni, Bw Lenolkulal amekana kutia kutia kibidoni Sh84 milioni naye Sonko alikana kufuja Sh381 milioni katika kesi mbili zinazomkabili.