2019: Sonko alivyotumia majina 5 kufanikisha ufisadi
Na RICHARD MUNGUTI
KESI ya ufisadi iliyomkumba Gavana wa Nairobi Mike Sonko aliyefikishwa kortini Desemba 9, 2019 ilifichua madai kwamba alitumia majina matano tofauti.
Alikabiliwa na mashtaka 18 ya ubadhirifu wa zaidi ya Sh381 milioni akitumia majina hayo kupokea pesa kutoka kwa kampuni saba zilizopewa kandarasi za kutoa huduma katika kaunti.
Uchunguzi uliofanywa na Tume ya Kukabili ufisadi nchini (EACC) na kuwasilishwa kortini na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji, ulionyesha kuwa Sonko alifungua akaunti 12 tofauti katika matawi ya Benki ya Equity Limited (EBL) akitumia majina haya matano.
Akaunti hizi za benki ya EBL ziko katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Kwale.
Majina hayo ni Kioko Mike Sonko, Mbuvi Gidion Kioko Mike Sonko, Mbuvi Gideon Kioko, Mike Sonko Mbuvi Gideon Kioko na Mbuvi Gideon Kioko Sonko.
Kampuni saba zilizopewa kandarasi katika kaunti ya Nairobi ni Web Tribe Ltd (iliyopewa kandarasi ya kukusanya ushuru, Yiro Enterprises, Hardi Enterprises Limited, Toddy Civil Engineering Limited, Arbab Auto Limited, ROG Security Limited na High Energy Petroleum Limited.
Katika kesi ya kwanza ya ufujaji wa Sh24,100,000 Sonko alishtakiwa pamoja Fredrick Odhiambo almaarufu Fred Oyugi mwenye kampuni ya Yiro Enterprises, Danson Muchemi, Robert Muriithi, Zablon Onyango na Antony Otieno Ombok almaarufu Jamal.
Katika kesi ya pili alishtakiwa pamoja na wafanyakazi wa kaunti Mabw Peter Mbugua Kariuki, Patrick Mwangangi, Wambua Ndaka, Andrew Nyasiego, Samuel Mwangi Ndungu, Edwin Kariuki Murimi na Preston Mwandiki Miriti. Walikana kufuja Sh357,390,229.95 za kaunti ya Nairobi.
Walishtakiwa kuwa walitekeleza uhalifu huu kati ya Julai 1, 2018 na Machi 2019.
Mnamo Januari 19 2019, Sonko alishtakiwa kwamba akiwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi kwa njia ya ufisadi alipokea Sh1 milioni kutoka kwa kampuni ya Web Tribe Limited iliyokuwa imepewa kandarasi ya kukusanya ushuru.
Hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Douglas Ogoti alielezwa kuwa Sonko alipokea pesa hizo katika akaunti ya EBL tawi la Nyali, Mombasa. Jina alilotumia katika akaunti hiyo ni Mike Sonko Mbuvi Gidion Kioko.
Shtaka hili lilisema pesa hizo ziliwekwa katika akaunti hiyo na Kampuni ya ROG Securities baada ya kuzipokea kutoka kwa kampuni ya Web Tribe Ltd.
Shtaka la tatu lilisema Gavana huyu alipokea Sh1m Januari 19, 2019 katika akaunti ya EBL tawi la Kenyatta Avenue iliyofunguliwa kwa jina la Mbuvi Gideon Kioko Sonko
Siku hiyo hiyo gavana huyu alidaiwa kupokea Sh1 milioni zilizotumiwa kampuni ya ROG Securities na Gigiri.
Katika tawi la Fourways la EBL akitumia jina la Mike Sonko Mbuvi Gideon Kioko, mshtakiwa huyu alipokea Sh1m.
Pesa hizo zilitumwa na Fredrick Odhiambo almaarufu Fred Oyugi kwa kampuni ya ROG Securities kutoka kwa kampuni yake Yiro Enterprises.
Mnamo Desemba 28 2018 Sonko alipokea Sh1 milioni katika akaunti yake iliyoko katika benki ya EBL tawi la kaunti ya Kwale akitumia jina Mike Sonko Mbuvi Gideon Kioko.
Sonko ameshtakiwa kupokea kwa njia ya ufisadi zaidi ya Sh40 milioni.