Habari MsetoSiasa

2022: Tangatanga walivyopanga kadi zao kumzima Raila

November 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na COLLINS OMULO

NAIBU Rais William Ruto na viongozi wa Chama cha Jubilee wanaoegemea upande wake, maarufu kama Tangatanga, wamepanga mikakati thabiti ya kumnyamazisha kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi hao wanamchukulia Bw Odinga kama hasimu mkuu wa Bw Ruto katika kinyang’anyiro cha 2022 na hivyo wamejitwika jukumu la kulemaza juhudi zake zote zinazolenga kujipigia debe kuwa rais.

Wakizungumza kwenye hafla ya kutoa shukrani kwa mgombea wa Jubilee, Kibra McDonald Mariga mnamo Ijumaa, walipuuzilia mbali tishio lolote kutoka kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula katika uchaguzi wa urais 2022.

Mpango wao ni kumsawiri Bw Odinga kama mchochezi wa ghasia na ukatili huku ODM, chama atakachotumia kuwania urais, kikisawiriwa kama kundi la kigaidi na wala sio chama cha kisiasa.

Kwa upande mwingine, Dkt Ruto atasawiriwa kama kiongozi mzalendo anayependa taifa na ambaye amejumuisha jamii zote katika juhudi zake za kuunganisha taifa.

Katika hafla hiyo, Naibu Rais Ruto alitumia zaidi ya dakika 20 akizungumza kuhusu uchaguzi mdogo wa Kibra mnamo Novemba 7, na jinsi ODM ilivyowashambulia kikatili viongozi na wafuasi wa Jubilee huku akisawiri chama hicho na viongozi wake kama kundi la wanamgambo wanaonawiri katika ghasia wanaposaka mamlaka ya kisiasa.

Dkt Ruto alisimulia jinsi viongozi na wafuasi wa Jubilee walivyotendewa ukatili huku akishutumu ODM na viongozi wake dhidi ya kuendelea kuamini siasa za kikatili kama njia ya kupata mamlaka akiwakumbusha kwamba enzi ambazo uchaguzi ulifanywa kupitia vitisho na ukatili zimepita.