Familia ya aliyeliwa na fisi yataka fidia kutoka kwa serikali
Na LAWRENCE ONGARO
FAMILIA moja katika kijiji cha Ndarugu-Komo, Kaunti ya Kiambu, inalilia haki baada ya mwanamume mmoja katika familia hiyo kuliwa na fisi.
Bw Joseph Njuguna Kamau aliyekuwa na umri wa miaka 64 alipokumbana na mauti, aliliwa na fisi mwaka wa 2017 na hadi leo familia hiyo haijapata haki kutoka kwa serikali.
Bw Fredrick Kahuha, 50, ambaye ni nduguye marehemu alisema Jumatano wamejaribu kuzunguka afisi za serikali bila mafanikio yoyote.
Cha kushangaza wengi ni kwamba familia hiyo imehifadhi mifupa ya marehemu kwenye nyumba yao huku wakingoja mwelekeo kutoka kwa serikali.
Kulingana na Bw Kahuha, marehemu aliliwa na fisi Machi 2017 baada ya kuvamiwa akiwa na ng’ombe malishoni.
“Sisi tulikosa kumuona ndugu yetu jioni hiyo, lakini tuliona ng’ombe wanane waliokuwa malishoni wakirejea bomani. Baada ya kumtafuta siku iliyofuata, tulipata mifupa na vipande vya nguo alizokuwa amevalia siku ya mkasa,” alisema Bw Kahuha.
Alisema walipiga ripoti kwa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) na polisi wakati mmoja.
Baadaye waliarifiwa waandikishe taarifa.
Kulingana naye ni kwamba polisi waliwaarifu wahifadhi mifupa hiyo huku fuvu la kichwa likipelekwa katika maabara ya serikali jijini Nairobi kufanyiwa uchunguzi wa DNA.
Alisema tangu wakati huo wamekuwa wakingoja matokeo kamili ya matokeo hayo ili kudhibitisha ukweli wa mwili huo.
Anasema linalowakera zaidi ni kwamba mama yao amekuwa akihifadhi mifupa hiyo chumbani kwa karibu miaka mitatu sasa.
Katika kituo cha polisi cha Munyu Police Patrol Base walijaza taarifa katika kitabu cha matukio OB 13/26/3/2017.
Baadaye pia waliandikisha taarifa katika Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) waliandika ripoti nambari OB 07/28/7/2017.
Mamake marehemu, Bi Margaret Njeri Kamau, 80, alisema anasumbuliwa na jinamizi kila mara anapoona mifupa hiyo kwenye chumba chake.
“Tayari nimekabiliwa na maradhi mengi mwilini kutokana na kupotea ghafla kwa mwanangu mpendwa – aliyekuwa nguzo kuu – katika familia hii. Marehemu alifanya kazi zote za boma kama kulisha mifugo, kuteka maji, na hata kwenda shambani kulima,” alisema Bi Kamau.
Wakazi wa eneo hili wanadai ya kwamba kwa chini ya miaka mitatu sasa watu wengine watatu wameliwa na fisi hao ambao ni wengi ajabu katika kijiji hicho.
“Fisi hao huonekana katika vikundi vya wanyama 10 na hata zaidi. Hata watoto wa shule husindikizwa na wazazi wao shuleni asubuhi wakihofia wao kuvamiwa na fisi hao,” alisema Bw William Kariuki, 80, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.
Wanasema ng’ombe 10, na mbuzi 20 wameliwa na fisi hao kwa muda wa mwaka mmoja uliopita.
Wanaitaka serikali, kupitia KWS, kufanya juhudi kuwatoa fisi hao ambao huonekana kutoka saa 12 za jioni wakizurura ovyo vijijini.