Habari Mseto

Gretsa kupanua chuo katika ardhi ya ekari 60

December 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuzingatia maswala ya utafiti na teknolojia mpya katika vyuo vikuu ili kuambatana na mambo ya kisasa.

Chansela wa Chuo cha Gretsa mjini Thika Dkt Kibathi Mbugua alisema hayo na kuongeza kuwa chuo hicho kina mipango ya kupanuliwa huku wakitarajia kuhamia eneo la Makuyu katika kaunti ya Murang’a.

Alisema chuo hicho kinatarajiwa kujengwa katika shamba la ekari 60 huku wakipanga kujenga kituo kikubwa cha utafiti cha kisasa.

“Umefika wakati kuona ya kwamba tunapanua chuo chetu kutoka mji wa Thika hadi Murang’a ili kujiendeleza kwa njia ya kipekee,” alisema Dkt Mbugua.

Alisema chuo hicho cha Gretsa kilizinduliwa mara ya kwanza miaka kumi iliyopita ambapo wahitimu wapatao 7,000 wamepitia chuo hicho.

Alisema hayo mnamo Jumatano wakati wa kufuzu kwa wahitimu wapatao 600 katika katika shahada tofauti.

Aliwahimiza wahitimu hao kuwa kielelezo chema katika jamii na wawe watu wa kujituma na kubuni ajira wenyewe..

“Huu sio wakati wa kutegemea kutendewa kila kitu lakini ni vyema kuonyesha ujasiri na kuendesha mambo yako mwenyewe,” alisema Dkt Mbugua.

Alisema tayari wametenga zaidi ya Sh 100 milioni za kupanua chuo hicho eneo la Makuyu.

Profesa Francis Kibera ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho aliwashauri wahitimu hao kufanya juhudi kugeuza maisha yao kwa kujitafutia mwelekeo wao.

“Ninatoa mwito kwa kaunti ya Kiambu kufanya juhudi kuona ya kwamba vijana wetu kadha kutoka chuo hiki wanapata ajira huko,” alisema Prof kibera.

Alihimiza wahitimu hao wawe mstari wa mbele kuyonyesha ya kwamba wanao uwezo wa kuonyesha ya kwamba wanao uwezo wa kuonesha ujuzi wao.

“Wakati wote usiharibu muda wako mwingi kutenda mambo yasiyo na maana na mjiepushe na kuingia katika mtego ya kutenda maovu. badala yake jitume na uonyeshe kuwa masomo ulioyasoma ni muhimu wakati wowote,” alisema msomi huyo.

Aliwasihi wasikubali kuingia kwenye mitego ya kutumia madawa za kulevya na kujiunga na vikundi vibaya .

“Kila mmoja wenu ana nafasi yake ya kujiamulia mambo yake mwenyewe na ni sharti uwe na mwelekeo ufaao,” alifafanua.

Dkt Margaret Mbugua ambaye mmoja wa mwenyekiti wa kamati ya bodi ya chuo hicho aliwahimiza wazazi waliofika katika hafla hiyo wawe mstari wa mvbele kuwapa mawaidha wana wao hasa wakati huu tunapoenda katika likizo ndefu ya krisimasi.

“Nyinyi wazazi ni sharti muwe mstari wa mbele kuwaongoza watoto wenu wawe na tabia njema. wakati huu tupo katika wakati mgumu ambapo vijana wanafanya maovu bila kutafuta ushauri kutoka kwa wataalam,” alisema Dkt Mbugua.