Masharti kwa wanachama wapya wa NHIF
Na BENSON MATHEKA
SHIRIKA la Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) limetoa masharti makali kwa wanachama wapya kuanzia mwezi huu, ambayo lazima watimize kabla ya kulipiwa bili za matibabu wakiugua.
Miongoni mwa masharti hayo ni kusubiri kwa siku 90 baada ya kusajiliwa pamoja na kulipa ada za mwaka mmoja bila kuchelewa, ili mtu aweze kupata huduma za bima.
Bodi ya shirika hilo ilisema masharti hayo yanalenga kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (UHC) na kuhakikisha kuwa wanadumisha wanachama.
“Bodi imependekeza kuwa, muda wa wanachama wapya kusubiri kabla ya kunufaika na bima uwe siku 90 badala ya siku 60. Pia watatoa malipo ya mwaka mmoja, ambayo yanapaswa kukamilika katika kipindi cha kusubiri bila kuchelewa, kabla yao kunufaika,” ilisema barua ya Katibu wa Bodi kwa wakuu wote wa usajili katika matawi yote nchini.
Mwanachama akichelewa kulipa ada za kila mwezi kwa miezi 11, atakuwa akitozwa faini ya asilimia 50 ya ada ya kila mwezi. Pia, atatakiwa kulipa ada za mwaka mmoja kwa mpigo na kupigwa marufuku dhidi ya kupata huduma kwa siku 30.
Mwanachama atakayechelewa kuwasilisha malipo kwa mwaka mmoja atalazimika kujisajili upya, na atanufaika na bima hiyo baada ya miezi mitatu, yaani siku 90.
Aidha, atalazimika kulipa ada za mwaka mmoja kwa mpigo huku akitozwa faini ya asilimia 50 ya ada za kila mwezi.
Kwa wanaojilipia ada zao wenyewe, NHIF itakuwa ikilipia huduma za kujifungua miezi sita baada ya wanachama kutimiza masharti yaliyowekwa, sawa na wanaohitaji huduma maalum za matibabu.
“Kwa huduma za kujifungua na matibabu maalum, mtu anayetumia kadi ya mwanachama atakuwa akisubiri kwa miezi sita. Isipokuwa watoto wanaozaliwa mradi tu waorodheshwe miongoni mwa wanaopaswa kunufaika na kadi ya mwanachama,” inaeleza barua hiyo ya bodi kwa wakuu wa usajili na teknolojia wa NHIF.
Mwanachama akiongeza watoto wapya katika orodha ya wanaopaswa kunufaika na kadi yake, watakuwa wakisubiri kwa siku 30 kulipiwa bili ya hospitali na NHIF, iwe wamelazwa hospitalini au wametibiwa na kurudi nyumbani.
Chini ya masharti hayo mapya, kwa wanachama wa kitaifa (yaani, wafanyakazi wa serikali kama walimu na polisi) ni mchumba mmoja tu (mume au mke) na watoto watano watakaolipiwa bili ya matibabu na NHIF kuanzia mwaka huu.
Mtu akitaka kuongeza idadi ya watoto au wachumba, atakuwa akilipa ada ya zaidi atakazofahamishwa baada ya maafisa wa NHIF kukagua ombi lake.
Wazee, walemavu na wanachama chini ya mpango wa Linda Mama na Inua Jamii hawataathiriwa na masharti hayo.