Afanya KCPE akiwa ndani baada ya kuchoma nyumba ya mamake
Na PETER MBURU
MTAHINIWA wa mtihani wa KCPE kutoka kaunti ya Bomet anafanyia mtihani katika kituo cha polisi, baada ya kukamatwa kwa madai ya kuchoma nyumba ya mamake.
Mvulana huyo wa miaka 19 na ambaye alijisajili kama mtahiniwa wa kibinafsi kutoka kijiji cha Kelyot alikamatwa Jumanne jioni na anazuiliwa pamoja na mtu mwingine wa familia yake ambaye wanadaiwa kushirikiana kutekeleza uovu huo.
Mkuu wa polisi kaunti hiyo alidhibitisha kuwa mwanafunzi huyo anaendelea kufanyia mtihani huo wa kitaifa, ambao unakamilika leo, katika kituo cha polisi.
“Mtahiniwa huyo anafanyia mitihani katika kituo cha polisi baada ya kukamatwa kuhusiana na tukio la uteketezaji nyumba kijiji cha Kelyot, Bomet ya Kati,” akasema Bw Samson Rukunga, OCPD wa eneo hilo.
Bw Rukunga alisema kuwa punde akikamilisha mitihani, mtahiniwa huyo atafikishwa kortini na kufunguliwa mashtaka mara moja.
Mkurugenzi wa elimu kaunti ya Bomet Mabale Indiatsi alithibitisha kuwa mtahiniwa huyo alifanyia mitihani ya masomo ya Sayansi, Kiswahili na Insha katika kituo hicho cha polisi Jumatano.
“Alikuwa mmoja wa watahiniwa 27 waliosajiliwa kufanyia mtihani katika kituo cha mitihani cha shule ya msingi ya Bomet lakini sasa alifanya mitihani ya Jumatano akiwa polisi, ambapo anatarajiwa kufanya ule wa Alhamisi na ambao ni wa mwisho,” akasema Bw Indiatsi.