Afisa wa KDF akana kukopeshwa Sh1.3m
Na RICHARD MUNGUTI
AFISA wa KDF alishtakiwa Jumanne kwa kosa la kughushi barua na kupokea mkopo wa Sh1.3 milioni kutoka kwa benki ya Standard Chartered.
Boniface Omondi Onyango alikabiliwa na mashtaka mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi
Shtaka la kwanza lilisema kuwa mnamo Februari 22, 2019 akiwa na nia ya kulaghai alighushi taarifa ya benki ya Cooperative tawi la Aga Khan Walk ikionyesha kiwango cha pesa alicho nacho katika akaunti yake.
Shtaka liliendelea kusema alighushi taarifa hiyo ya benki kwa lengo la kuilaghai idara ya kijeshi DoD.
Shtaka la pili lilisema kuwa mnamo Machi 5 katika benki ya SCB alipokea Sh1.3milioni akidai barua aliyokuwa nayo imetoka kwa DoD imruhusu apokee mkopo huo.
Mahakama iliombwa imwachilie kwa dhamana kwa vile amekuwa amezuiliwa katika kororkoro ya DoD tangu Mei mwaka huu.
“Mshtakiwa aliachiliwa Jumatatu ndipo akafikishwa kortini baada ya kutimuliwa kazini na kupewa nguo za raia,”hakimu mkuu Francis Andayi alifahamishwa.
Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000.