Afisa wa polisi akana kumuua mahabusu
Na RICHARD MUNGUTI
AFISA wa polisi alikiri katika mahakama kuu Jumatatu mahabusu anayeshukiwa aliteswa akiwa seli alimwona akiwa amelowa maji.
Bw Kennedy Simiyu alimweleza Jaji Stella Mutuku kwamba aliyekuwa msimamizi wa kituo cha polisi cha Ruaraka hakumpiga na kumjeruhi mahabusu huyo Martin Koome akiwa ndani ya seli.
Bw Simiyu aliyekuwa akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili afisa huyo mkuu wa polisi Nahashon Mutua alisema katika kituo cha polisi cha Ruaraka kuna tangi la maji na kwamba “Koome hakutoswa mle na mshtakiwa (Mutua).
Jaji Mutuku alifahamishwa kwamba Koome aliyekuwa ameshambuliwa na wanakijiji kwa madai alijaribu kumuua mtoto wake alikufa saa chache baada ya kupelekwa Hospitali Kuu ya Kenyatta.
Alifikishwa katika kituo cha polisi cha Ruaraka kutoka kijiji cha Baba Dogo.
Shahidi huyo aliambia mahakama kwamba Koome alipigwa na mahabusu wenzake.
Kabla ya kukamatwa na kushtakiwa kwa Bw Mutua, mahabusu kwa jina Kelvin Odhiambo almaarufu Boxer alikuwa ameshtakiwa kisha akaachiliwa huru.
Hatimaye Bw Mutua alishatkiwa baada ya mamlaka ya utendakazi wa polisi (IPOA) kuchunguza kisa hicho.
Koome anadaiwa alipigwa na kuuawa ndani ya seli katika kituo cha Ruaraka mnamo Desemba 19, 2013.
Alipopelekwa KNH polisi walisema marehemu alikuwa amepigwa na umati wa watu. Marehemu alikuwa amevimba kichwani na hata ilikuwa vigumu kwa mkewe kumtambua.
Bw Mutua amewaita mashahidi watano kufikia sasa katika jitihada za kujinasua.
Mahakama iliambiwa marehemu aliteswa hadi akafa alipokuwa anazuiliwa katika kituo hicho cha polisi cha Ruaraka.