Habari MsetoSiasa

Afisi ya DPP yachunguzwa kwa ulaji rushwa

June 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji amekiri kuwa uchunguzi unaendeshwa katika afisi yake kuhusiana na sakata ya ulaji rushwa miongoni mwa maafisa wake.

Hii ni kufuatia kukamatwa kwa mwendesha mashtaka mmoja katika mahakama moja ya Taita Taveta kwa madai ya kupokea hongo ya Sh30,000 ili kushawishi kesi fulani ambayo alikuwa akiishughulikia.

“Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) angependa kujulisha umma kwamba Afisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) inaendesha uchunguzi katika Afisi ya DPP kuhusiana na madai uhalifu wa kifedha,” afisi yake ilisema kupitia twitter huku ikithibitisha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa mashtaka.

“DPP ana habari kuhusu operesheni iliyoendeshwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) katika mahakama ya Taita Taveta iliyopelekea kukamatwa kwa kiongozi mmoja wa mashtaka kwa madai ya kupokea mlungula. DPP atachukua hatua ya kisheria uchunguzi utakapokamilishwa,” taarifa nyingine ya Twitter ikasema.

Afisa huyo, Donald Omondi, alikamatwa baada ya kuchukua hongo hiyo ili kushawishi kesi dhidi ya mshtakiwa wa uuzaji wa pombe haramu kutoka nchi ya Tanzania.

Duru za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa afisa huyo alimuahidi mshtakiwa kuwa atapunguziwa adhabu ya shtaka lake hadi Sh20 000 ikiwa angetoa hongo ya Sh40 000.

“Inadaiwa kuwa alisema kuwa pesa hizo zingegawiwa hakimu aliyekuwa akisikiza kesi hiyo,” akasema mdokezi wetu.

Mshtakiwa huyo alipiga ripoti kwa tume hiyo ambapo afisa huyo alikamatwa alipopokea pesa hizo katika jumba la mahakama hayo.

Akithibitisha kisa hicho, Mkuu wa Polisi wa kaunti hiyo Bi Halima Abdi alisema kuwa afisa huyo alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Taveta.

Alisema mshukiwa atafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka ya ulaji rushwa na pia matumizi mabaya ya afisi ya umma.

“Kwa sasa uchunguzi ungali unaendelea ili kupata ushahidi zaidi,” akasema Bi Abdi.

Afisa huyo aliachiliwa kwa dhamana ya Sh50 000 pesa taslimu akingojea kufikishwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi mjini Mombasa mnamo Juni 7, 2018.