AFLATOXIN: Mbunge ataka maafisa wa KEBS wakamatwe
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imeombwa kukamata maafisa wa Idara ya Ubora wa Bidhaa (KEBS) kwa kushindwa kuzuia unga wa mahindi wenye sumu ya aflatoxin kuuzwa madukani.
Wakenya wa matabaka mbalimbali wamelalamika kuwa maafisa wa KEBS wamewakosea Wakenya kwa kuwaweka katika hatari ya kupata magonjwa kama vile saratani kwa kutumia vyakula ambavyo havijafikia ubora unaostahili.
Mwakilishi Mwanamke katika Kaunti ya Kakamega, Bi Elsie Muhanda, alisema maafisa hao ndio wenye jukumu la kukabidhi viwanda vya usagaji unga kibali baada ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.
Wiki iliyopita KEBS ilipiga marufuku uuzaji wa unga chapa Starehe, Kifaru, Dola, 210 na Jembe.
Bi Muhanda anataka serikali ifuatilie suala hilo ili Wakenya wafafanuliwe jinsi unga wenye sumu ulivyoachiliwa kufika hadi manyumbani mwao kupitia madukani kabla KEBS kuagiza bidhaa hizo ziondolewe.